Rais Kikwete akutana na viongozi wa chama cha Albino Tanzania ikulu jijini Dar es Salaam. - LEKULE

Breaking

5 Mar 2015

Rais Kikwete akutana na viongozi wa chama cha Albino Tanzania ikulu jijini Dar es Salaam.




Kikao cha Rais na watu wenye ulemavu wa ngozi Albinism almanusura kivunjike baada ya walemavu hao kuhamishia mgogoro wao wa uongozi ikulu na kusababisha vurugu iliyopelekea watolewe nje ya jengo la ikulu na baadae kuanza kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Mapema asubuhi walemavu hao walifika eneo la mapokezi ikulu ambapo waliokuwa wameorodheshwa kwa ajili ya kuonana na rais waliakikiwa majina yao lakini likajitokeza kundi lingine ambalo halikuwa kwenye orodha muda wa waliotakiwa kuingia ndani ulipowadia ndipo vurugu zikaanza za kuwazuia viongozi hao wasiingie ndani bila wao kwa madai kuwa kwa sasa hawana viongozi.

Tafrani hiyo iliendelea kwa muda na kusabisha shughuli zote za mapokezi kusimama kutokana na kelele zilizosababishwa na walemavu hao hali iliyosababisha askari waliokuwa eneo hilo kuingilia kati na kuanza kuwasihi watoke nje ya geti wakajipange upya huku baadhi yao wakieleza kusikitishwa na kitendo hicho na kwamba kimewatia aibu.

Mara baada ya kutoka nje ya geti la ikulu walianza kurushiana maneno wao kwa wao na waandishi wa habari walipotaka kuzungumza na mwenyekiti waliyemkataa kwa madai kuwa uongozi wake uliisha mwishoni mwa mwaka jana kundi hilo lilitokea tena na kuanza kumzomea hali iliyosababisha ashindwe kuendelea na mahojiano na hapo ndipo ngumi zikaanza.

Maafisa usalama walifanikiwa kumuokoa mwenyekiti huyo ambapo baada vurugu kutulia askari aliyevalia sare alisikika akiwasihi walemavu hao kuondoka eneo hilo kwa amani huku baadhi yao wakielezea sababu za kuwazuia viongozi hao kwenda kuonana na rais.

Hata hivyo baada ya kundi hilo kuondoka eneo hilo majira ya mchana mwenyekiti huyo alirudi tena ikulu na kufanya mawasiliano na wenzake waliokuwa kwenye orodha ya kuonana na rais Kikwete na kufanikiwa kuonana naye.

No comments: