MKUTANO MKUU WA TFF WAANZA LEO HUKO MOROGORO - LEKULE

Breaking

14 Mar 2015

MKUTANO MKUU WA TFF WAANZA LEO HUKO MOROGORO


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) leo linafanya Mkutano Mkuu wa Mwaka mjini Morogoro kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Morogoro, ukiwa ni wa kwanza tangu uongozi mpya ulio chini ya Jamal Malinzi uingie madarakani 2013.

Mkutano huu unafanyika kwa siku mbili na unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe takribani 100 kutoka mikoa wanachama wa shirikisho hilo.
Wajumbe watakaowakilisha mikoa ni Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu kutoka kila mkoa.

Pia kutakuwepo wawakilishi wa klabu na wajumbe wengine kutoka vyama wanachama wa TFF ambavyo ni Chama cha Waamuzi (FRAT), Chama cha Makocha (TAFCA), Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMAna Chama cha Wachezaji (SPUTANZA).

 Ajenda za mkutano huo ni kufungua mkutano, uhakiki wa wajumbe, kuthibitisha ajenda, kuthibitisha muhtasari wa Mkutano Mkuu uliopita na yatokanayo na mkutano uliopita.
Nyingine ni hotuba ya Rais, ripoti kutoka kwa wanachama, kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji, kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013.

Pia kutakuwepo na agenda ya kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu, kupitisha Bajeti ya 2015, marekebisho ya Katiba, mengineyo na kufunga mkutano.
Awali, mkutano huu ulikuwa ufanyike mkoani Singida, lakini ulihamishwa kutokana na mkoa huo kutokuwa na hoteli za kukidhi mahitaji ya wajumbe na gharama kuwa juu.

Mkutano huu unakuja wakati TFF ikikabiliwa na changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa soka nchini, likiwamo suala la ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inasimamiwa na Bodi ya Ligi ikileta mkanganyikokwenye klabu za ligi hiyo kwani imekuwa ikibadilika bila kutolewa sababu za msingi.

No comments: