MKE WA MTU AKUMBWA NA MAUTI - LEKULE

Breaking

3 Mar 2015

MKE WA MTU AKUMBWA NA MAUTI



MASKINI! Aneth Solomon (31), mkazi wa Manzese, Dar ambaye ni mke wa mtu, amekumbwa na mauti akiwa ameondoka nyumbani kwa kuaga anakwenda kuhani msiba ukweni kwake, Uwazi lina mkasa mzima.

Mwili wa Aneth uliokotwa Februari 21, mwaka huu kwa kukutwa kwenye bonde lililopo katikati ya Magomeni na Kinondoni Mkwajuni, Dar maarufu kwa jina la ‘Msitu wa Kifo’.

FAMILIA ILIVYOSEMA
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya familia ya marehemu zilisema kuwa, Aneth ambaye alikuwa ndani ya ndoa kwa miezi nane tu, alifika Magomeni kwa wazazi wake, Februari 14, mwaka huu na kumwambia mama yake mzazi kwamba anakwenda ukweni kulikokuwa na msiba siku chache zilizopita. Kutoka kwao na ukweni ni karibu.

“Siku hiyo aliondoka nyumbani kwa mama yake kama saa 12.30 jioni kuelekea ukweni. Hapana umbali mrefu unavuka bonde tu pale unatokea Kinondoni, nadhani marehemu aliamua kupita njia ya mkato inayopitia bondeni ili atokee ng’ambo badala ya kufuata barabara.

“Lakini baada ya muda, kule ukweni ambako alishapeleka taarifa kwamba anakwenda, walianza kupata wasiwasi baada ya Aneth kutotokea kwa muda aliousema.”

MAWASILIANO YAANZA
“Ukweni kwake, walilazimika kuwasiliana na upande wa mume, ambaye alidai mkewe alishaondoka na alishafika kwa mama yake, lakini mama mtu alipopigiwa simu, alizidisha wasiwasi baada ya kusema binti yake alishaondoka muda mrefu kuelekea ukweni,” alisema mmoja wa wanafamilia.Ndugu walianza kumsaka Aneth tangu Jumamosi ya Februari 14, mwaka huu hadi alipopatikana akiwa amekufa Alhamisi ya Februari 19.

WALIVYOSEMA WAKAZI WA BONDENI
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya jirani na ulipokutwa mwili huo walisema walianza kusikia harufu kali iliyokuwa ikitoka kwenye karavati lililopo eneo hilo la bonde.

NAYE BABA MKWE
“Ilibidi tufuatilie, baada ya kufika eneo la tukio tulikuta mwili ndani ya karavati, kuuangalia vizuri tulimtambua kuwa ni Aneth ambaye ni mkwe wangu yaani mke wa mwanangu,” alisema Augustine Albert ambaye ni baba wa mume wa marehemu. Mume hakuweza kuzungumza.

Uwazi lililokuwepo katika eneo la tukio wakati mwili huo ukiopolewa, liliambiwa na majirani kuwa wanakumbuka kusikia kelele za mwanamke aliyeomba msaada usiku wa Jumamosi inayodaiwa ndiyo marehemu aliaga kwenda ukweni.

MJUMBE ANENA
Mjumbe wa Shina Namba 35, Kinondoni Mwinjuma, Rashid Kilewa alisema sehemu ulipokutwa mwili wa Aneth si salama kwani hata mwaka jana, waliokota mwili wa mtu.Alitoa wito kwa jeshi la polisi kufanya doria sehemu hiyo kuanzia saa 12 jioni na kuendelea ili kunusuru maisha ya watembea kwa miguu.

No comments: