Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Alendoufonyi Abdi (pichani) mkazi wa Uduru Machame mkoani Kilimanjaro, amenusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kuokolewa na waumini wa kanisa moja jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la Kijenge Banana Kata ya Olorieni, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste la Yerusalemu Mpya, Liberty Shirima alisema walimnusuru mwanamke huyo asiuawe na wananchi waliokuwa na hasira kali.
Aidha, aliongeza kuwa wakati walipokuwa katika mkesha wa maombi usiku wa Jumanne wiki iliyopita kanisani kwao, walipigiwa simu na kutaarifiwa kulikuwa na mtu waliyemtuhumu kuwa ni mchawi amedondoka katika eneo lao.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, akiwa na baadhi ya waumini wake, saa tisa usiku waliondoka kanisani hadi eneo la Baghdad Kijenge na kumkuta mwanamke huyo akiwa amezungukwa na watu waliokuwa wakidai alikuwa mchawi.
“Walidai alidondokea eneo la shimo baada ya wenzake kumnyan’anya kijiko pamoja na kitambaa chekundu,” alisema Mchungaji Shirima Aliongeza kuwa, mwanamke huyo alikuwa akijieleza kwa shida akidai kuwa alitokea Kijiji cha Uduru Machame mkoani Kilimanjaro, walikuwa katika mizunguko ya kikazi ya kutafuta damu za watu.
Mwanamke huyo alipohojiwa na mwandishi wetu alisema wakiwa katika safari yao angani huku wamepanda juu ya mgomba wa ndizi, wenzake walimnyang’anya kijiko na kitambaa chekundu ndipo alipojikuta amedondoka chini. Polisi mkoani Arusha imethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo mwanamke huyo alipelekwa kituoni hapo kwa mahojiano zaidi.
No comments:
Post a Comment