Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid
amesisitiaza tamko la kupiga marufuku uvutaji wa sigara katika maeneo ya
umma ili kuilinda jamii kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa
sigara.
Tamko la Waziri limekuja ikiwa ni siku moja tu
baada ya maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, moja ya magonjwa
yanayosababishwa na uvutaji wa tumbaku.
Agizo hilo
limezingatia Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL,
ya mwaka 2003, Kipengele cha 12(1) ambacho kinakataza matumizi ya bidhaa
hiyo katika maeneo ya umma.
“Agizo hili linawataka
wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku, kupunguza au kuacha kabisa, pia
linaijumuisha jamii yote kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu
wa kuzuia uvutaji katika maeneo ya umma,” alisema Waziri katika tamko
lake.
Uvutaji sigara ulianza kupigwa marufuku kwa mara
ya kwanza mwaka 1575 na Kanisa la Katoliki lakini katika karne ya 20
harakati dhidi ya uvutaji sigara zilipamba moto kwa sababu za kiafya.
Sababu
kubwa ya kupiga marufuku ni ukweli kwamba uvutaji sigara ni hiari
wakati kuvuta pumzi ni lazima, hivyo mtu anayetumia kilevi hicho hana
budi kukaa mbali ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa kama ya moyo
na saratani kwa wasiotumia na ambao kuvuta pumzi ni lazima.
Msemaji
wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja alisema nia ya marufuku hiyo ni
kuhakikisha wizara inatimiza kwa vitendo sheria hiyo ya bidhaa za
tumbaku kwa kupiga marufuku na kuchukua hatua za kisheria. “Jamii
itusaidie kutoa elimu katika hili, kuna suala la kujenga maeneo maalum
ya kuvuta sigara na elimu kwa wale wanaovuta,” alisema.
Sheria
ya usimamizi wa bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003, inaeleza kuwa nia ni
kuwalinda vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 na wale wasiovuta
wasishawishike kuvuta.
Kuwalinda wasiovuta wasipate
madhara, kuifahamisha jamii juu ya madhara ya tumbaku na madhara ya
kuvuta moshi wa sigara inayovutwa na mwingine na kuhakikisha jamii haina
wavutaji sigara.
Maeneo ambayo yamepigwa marufuku
kuvuta sigara yametajwa katika tamko hilo kuwa ni katika ofisi zote za
serikali na taasisi zake, hospitali za umma, vyuo vikuu na shule za
umma, vituo vya usafiri wa anga, mabasi, bandari na treni, bustani,
fukwe na katika maeneo ya kupumzika ya umma.
Pia tamko hilo la wizara limekataza uvutaji wa sigara katika mikutano yote ya kiserikali.
“Wizara
inawataka wale wote ambao wanataka kuacha kabisa kuvuta sigara,
wawatafute wataalamu wa afya ili wapate ushauri wa kitaalamu,” alisema
waziri katika tamko hilo.
Kadhalika, agizo hilo
limewataka wafanyakazi wa sekta ya afya na watumishi wa umma kuhakikisha
wanafanyia kazi na wanasimamia agizo hili.
“Tunataka
kila mmoja ashiriki katika agizo hili la kuzuia bidhaa za tumbaku, sekta
binafsi, asasi za kidini na wadau wengine wa afya watusaidie katika
kufanikisha hili,” alisema Waziri
Wakati wizara ikitoa tamko hilo, Kampuni ya Sigara (TCCL) imekuwa moja ya kampuni zilizoongoza kwa kulipa kodi mwaka jana.
No comments:
Post a Comment