Lukuvi amsimamisha kazi ofisa ardhi - LEKULE

Breaking

15 Mar 2015

Lukuvi amsimamisha kazi ofisa ardhi


Kufuatia kukithiri kwa migogoro ya ardhi mkoani Mwanza, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemsimamisha kazi Ofisa Ardhi Manispaa ya Ilemela, Asubuhi Otieno.
Otieno anatuhumiwa kujipachika cheo cha kamishna ardhi mteule na kubadili hati miliki ya ardhi namba 147 Kitalu C, mali ya marehemu Almas Chande na kummilikisha Kabinga Mkama.
Pia, Ofisa Mipango Miji Nyamagana, Kazi Maduhu na Ofisa Ardhi wake, Sylvester Salvatory hatima yao inasubiri ushauri wa kamati iliyoundwa na Waziri Lukuvi kutokana na malalamiko mengi ya wananchi kuelekezwa kwa watumishi hao.
Uamuzi wa kumsimamisha Otieno ulifikiwa kwenye kikao cha majumuisho ya ziara ya siku tatu ya waziri huyo jijini Mwanza juzi.
Lukuvi aliunda kamati maalumu itakayochambua kwa mwezi mmoja barua za malalamiko 600 kutoka Manispaa ya Ilemela, 800 za Nyamagana na kumpa ushauri.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kusimamishwa kwa Otieno, mama mzazi wa marehemu Chande, Amina (78) aliwasilisha barua ya Desemba 17, 2013 ikimtaarifu kubadilika kwa mmiliki wa ardhi kutoka kwa Chande kwenda kwa Mkama.
Hali hiyo ilimshtua Lukuvi na kulazimika kumhoji ofisa huyo kama anaitambua barua hiyo.
Otieno alikiri kufanya hivyo na akatakiwa kuisoma mbele ya hadhara na yeye akaisoma kinyume na ilivyoandikwa.
Waziri Lukuvi hakuridhika ikabidi aisome mwenyewe na kukuta kilichosomwa ni tofauti na kilichoandikwa. Otieno alipoulizwa sababu za barua hiyo kutokuwa na muhuri wa kamishna, alikosa majibu na kusababisha umati wa watu kumzomea huku wakisema: “Bora umefika mwenyewe acha uyaone”.
Kuhusu Manispaa ya Nyamagana, Sylvester Salvatory anadaiwa kuvamia kiwanja cha Ester Jerome chenye namba 137 Kitalu X eneo la Kapripoint na kukiuza kwa mtu mwingine, huku akimwomba mmiliki halali Sh1 milioni ili amsaidie kukirejesha mikononi mwake.
Pia, Salvatory anadaiwa kumwomba Ester Sh300,000 kwa ajili ya kumpelekea Ofisa Mipango Miji, Kazi Maduhu ili amsaidie kumpatia hati miliki nyingine na kwamba, alimpa fedha hizo na kuahidiwa kupelekewa stakabadhi ambazo hajakabidhiwa hadi sasa.
Maelezo hayo yalimfanya Waziri Lukuvi kumsimamisha Salvatory na kumhoji tena kama anakifahamu kiwanja hicho, naye alikiri kukifahamu lakini akashindwa kutoa sababu za kumtoza fedha bila kumpatia stakabadhi mama huyo.
“Natetemeka kwa sababu ya ukweli, naona unaniuliza maswali ya kunionea, kama ni kuwajibika nitawajibika kwani sikuzaliwa kuwa Ofisa Ardhi Mwanza, ifahamike kuwa maisha ni popote,” alisema Salvatory huku akibubujikwa machozi.
Waziri Lukuvi alisema Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa migogoro ya ardhi, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza. Alisema migogoro hiyo inasababishwa na maofisa ardhi ambao aliapa kuwashughulikia.
Kikao hicho kilishirikisha zaidi ya wenyeviti 200 wa Jiji la Mwanza, kila mmoja aliwasilisha kabrasha lenye malalamiko kwenye mitaa yake.

No comments: