Klabu ya soka ya Chelsea imetawazwa kuwa mabingwa wapya wa kombe la Capital one baada ya kuishushia kichapo cha mabao 2-0, timu ya Tottenham katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Wembley Jumapili jioni.
Katika kipute hicho vijana wa kocha mwenye maneno mengi Jose Mourinho waliandika bao la kwanza katika dakika ya 45 ya mchezo huo kupitia kwa nahodha wake John Terry, bao hilo lilidumu mpaka timu hizo zilipokwenda mapumziko.
Katika kuthibisha kuwa siku ya kufa nyani miti yote huteleza, dakika ya 56 mlinzi wa Tottenham Kyle Walker aliwahakikishia vijana wa darajani ushindi wa kishindo baada ya kujifunga katika harakati za kuokoa hatari kutoka langoni mwake.
Kombe hili ni la kwanza kwa kocha Mourinho tangu ajiunge kwa mara nyingine klabuni hapo mwaka 2013 akitokea nchini Hispania alikokuwa akiifundisha miamba ya soka nchini humo Real Madrid.
No comments:
Post a Comment