BODI YA LIGI YAWAJIBU YANGA KUHUJUMIWA MECHI - LEKULE

Breaking

5 Mar 2015

BODI YA LIGI YAWAJIBU YANGA KUHUJUMIWA MECHI


Muda mfupi baada ya uongozi wa Yanga SC kudai kuhujumiwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), bodi hiyo imewajibu wanajangwa kwamba “mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu.”

Mapema leo, uongozi wa Yanga SC umetishia kutoingiza timu uwanjani katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu Stars iliyopangwa kuchezwa Uwanja wa Taifa Machi 11, kutokana na kile ulichodai kutoshirikishwa katika uamuzi wa mabadiliko ya ratiba.

Jery Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, amesema jijini hapa leo kuwa uongozi wa Yanga SC ulikuwa unatambua kwamba kikosi chake kingecheza dhidi ya JKT Ruvu kesho kabla ya kuivaa Simba SC Jumapili, lakini kimeshangaa baada ya kusoma kwenye mitandao kwamba mechi yao dhidi ya JKT Ruvu Stars haipo KESHO.
Hat hivyo, Fatma Shibo, Kaimu Ofisa Mtendaji wa TPLB, amesema mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara hayajafanywa kwa siri na yametokea kutokana na ushiriki wa timu nne za ligi hiyo, Azam FC, Mtibwa Sugar FC, Simba SC na Yanga SC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu.

Fatma amekanusha madai ya Yanga SC kwamba mechi yao dhidi ya JKT Ruvu Stars wanayodai ilipangwa kuchezwa kesho kwamba yamefanywa kwa siri, kwa vile uongozi wa wanajangwani ulitaarifiwa tangu Febuari 16 juu ya mabadiliko ya ratiba ya ligi.

“Mabadiliko ya ratiba ya ligi kuu yametokea kutokana na ushiriki wa timu nne za Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari mwaka huu,” Fatma amesema.

“Hili la pili la Yanga kudai hatukuwashirikisha katika kupangua mechi yao dhidi ya JKT Ruvu si kweli kwa sababu tuliwasiliana na uongozi wa Yanga tangu Februari 16. Labda wawe na tatizo la kutofungua email, lakini Katibu Mkuu wao (Jonas Tiboroha) alisema aliona email yetu kuhusu suala hilo,” amesema zaidi Fatma.

Ofisa huyo amesema bodi haina njama zozote za kuihujumu Yanga SC katika mechi zake kwani waliibeba pia katika kuilazimisha Tanzania Prisons FC irejeec Mbeya kutoka Dar es Salaam kucheza dhidi yao mechi waliyoshinda 3-0 jijini Mbeya juzi.

“Kama ni watu wa kulalamika, walipaswa kulalamika Prisons kwa sababu walikuwa hapa Dar es Salaam, lakini tukawaambia warejee kwao Mbeya kucheza dhidi ya Yanga baada ya uongozi wa Yanga kutuomba wacheze mechi zao zote zsa Mbeya kabla ya kwenda Botswana.

“Mpaka sasa bodi inadaiwa pesa ya gharama za usaffiri na timu ya Prisons kwa sababu tuliwafanya wasafiri mara mbili kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kurudi tena hapa Dar es Salaam,” amesema zaidi Fatma.

Katika hoja zake, Muro amedai TPLB ni janga la kitaifa na kwamba kusogezwa mbele kwa mechi hiyo dhidi ya kikosi cha Felix Minziro cha JKT Ruvu, ni hujuma dhidi ya Yanga SC, kwa kuwa timu hiyo ya Jangwani jijini hapa itakuwa na siku mbili tu za kupumzika baada ya kucheza dhidi ya maafande hao kabla ya kuivaa Platinum ya Zimbabwe katika mechi yao ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika Jumamosi.

Huku akihoji kiwango cha elimu cha Kaimu Ofisa Mtendaji wa TPLB, Fatma na watendaji wengine wa bodi hiyo, Muro amesema tayari uongozi wa Yanga SC umewasilisha barua TFF tangu jana kusaka ufafanuzi wa mabadiliko ya ratiba hiyo.

“Kwa sasa mpinzani wetu ni Azam FC na siyo Simba, mechi dhidi ya Simba kwetu ni kwa sasa kama bonanza, siyo kipaumbele chetu, sisi tunawasubiri siku hiyo ifike tucheze nao, lakini hawana jipya kwa tunawazidi pointi nyingi,”ametamba Muro.

“Azam kesho na keshokutwa tunamwacha mbali maana mpaka sasa tuko mbele yake kwa pointi nne katika msimamo wa ligi, sisi wapinzani wetu na klabu ambazo unaweza kuzilinganisha na sisi ni Kaizer Chief ya Afrika Kusini au TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambazo zinacheza michuano ya kimataifa,” amesema zaidi Muro

No comments: