WAZIRI
Mkuu, Mizengo Pinda amepiga marufuku watoto wa vigogo wa serikali,
mashirika binafsi, taasisi , madiwani na wanasiasa wengine kupewa
vizimba vya biashara katika soko kuu la kisasa la Mwanjelwa mkoani humu,
kuruhusu waliounguliwa bidhaa kwenye soko la awali wapate nafasi.
Akihutubia
maelfu ya wananchi katika eneo la soko hilo kwenye halmashauri ya Mbeya
Mjini, baada ya kuweka jiwe la msingi, Waziri Pinda alisema, jengo la
soko hilo kubwa la kisasa litawafaa hata wafanyabiashara wadogo wenye
ulemavu wa viungo.
Alisema
litawafaa kwa sababu amelikagua na kuona lina miundombinu inayowajali
kuanzia kwenye ngazi, lifti hadi vyooni, hivyo, visitokee visingizio
wakanyimwa vizimba kwa madai ya kutoweza kupanda na kushuka kwenye soko
hilo, na sababu nyingine zisizo na mashiko.
“Ninaonya
mapema kuwa soko hili ni kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ambao ndio
waliounguliwa na soko wakati ule ilipotokea ajali ya moto na kupata
hasara kubwa kutokana na bidhaa zao kuteketea...”
“Itakuwa
dhambi kama wataacha kupewa kipaumbele wakati wa ugawaji wa vizimba
hivi, kwa sababu wao ndio hasa wanaostahili, ndipo kama itatokea kuwa
nafasi zinabaki, zigawiwe kwa wajasiriamali wadogo wengine kulingana na
maombi yao,” Pinda alisema.
Aliongeza
kuwa hategemei kuona watoto kama wa akina Mizengo Pinda, madiwani,
wanasiasa na watoto wa vigogo wengine wa serikali, taasisi na mashirika
wakipewa nafasi kwenye soko hilo.
Aliwataka
wafanyabiashara ndogo watakaopewa vizimba katika soko hilo, wasiviuze
kwa tamaa, bali watafute mitaji kuanzia sasa, ili wasishindwe kuvitumia
wakati litakapoanza kufanya kazi.
Kwa
mujibu wa Kaimu Mkuu wa Mkoa huu, Deodatus Kinawilo soko hilo
lililojengwa kwenye eneo la ukubwa wa ekari 4.7, kwa zaidi ya Sh bilioni
13, zilizokopeshwa na benki ya CRDB, linatarajiwa kuanza kazi Aprili
mwaka huu.
Hata
hivyo, kutokana na jinsi alivyoona maendeleo ya ujenzi huo na hatua
iliyofikiwa na mkandarasi wa ujenzi huo ambaye ni kampuni ya ujenzi
iitwayo Nandra Engineering Construction, Waziri Mkuu alisema yeye anatoa
hadi Juni mwaka huu, wafanyabiashara wadogo wawe wamekwisha ngia na
kuanza kufanya biashara.
Pia,
alikumbushia umuhimu wa kulipa kodi ya serikali na kusema kuwa ndio
itakayosaidia soko hilo lidumu kwa sababu fedha za kodi zinazokusanywa
kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali zinatumika kuboresha miundombinu
katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, zikiwemo barabara kuu
zitakazowasafirisha wanunuzi kutoka maeneo tofauti ya ndani na nje ya
Tanzania.
Wakieleza
ni kwanini ujenzi wa soko hilo haukukamilika kwa wakati kama
ilivyotakiwa awali, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza na Meya
wa Jiji , Athanas Kapunga walimweleza Waziri Mkuu kuwa ni kwa sababu ya
mgogoro uliotokea kati yao na mkandarasi aliyekuwa akijenga mwanzoni,
kufuatia kumkatishia mkataba wa ujenzi.
Katika
hatua nyingine, mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, aliwashawishi wanawake
wajiunge katika makundi kuanzisha biashara kubwa katika soko hilo,
itakayowainua kiuchumi.
No comments:
Post a Comment