Serikali Yasikitishwa na Uamuzi wa Vijana wa Jeshi la JKT Kutaka Kujiunga na Majeshi ya Nchi Jirani Endapo Hawatapewa Ajira - LEKULE

Breaking

22 Feb 2015

Serikali Yasikitishwa na Uamuzi wa Vijana wa Jeshi la JKT Kutaka Kujiunga na Majeshi ya Nchi Jirani Endapo Hawatapewa Ajira


SERIKALI imesema madai ya baadhi ya vijana waliohitimu katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuruhusiwa kujiunga na vikundi vya majeshi ya nchi jirani yanayopigana ni kukosa uzalendo na uaminifu kwa taifa.
 
Pia, kukiuka kiapo chao cha uaminifu kwa nchi yao na hakioneshi kwamba vijana hao wana nia njema na taifa hili huku ikiweka wazi kuwa itavichukulia hatua vyombo vya habari vilivyotumika kusema uongo kuhusu wahitimu hao (JKT) kudai Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliwaahidi kuwapa ajira wahitimu hao.
 
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene alisema hayo juzi wakati akitoa ufafanuzi wa serikali kuhusu madai ya baadhi ya wahitimu hao kutaka kuandamana kudai ajira Ikulu.
 
Alisema baadhi ya wahitimu hao walidai kutaka kufanya maandamano kudai ajira Ikulu kwa kisingizio hicho na taarifa kutolewa na vyombo vya habari bila kutaja mahali na tarehe walipokutana na Sefue.
 
Imesema habari hizo si za kweli kwani Sefue hajawahi kukutana na wahitimu hao au hata wawakilishi wao na vyombo vya habari vilivyotoa taarifa hiyo vilitakiwa kuwasiliana na Katibu Mkuu kiongozi.
 
Alisema serikali imesikitishwa na madai ya vijana hao kwamba hawawezi kupatiwa ajira serikalini basi waruhusiwe kujiunga na majeshi ya nchi jirani yanayoshiriki katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
 
Alisema tangu kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT mwaka 2001 hadi 2014 vijana 104,594 wamejiunga na JKT wavulana wakiwa 76,832 na wasichana 27,762.
 
Alisema katika mwaka 2003 hadi 2-14 vijana 24,708 waliajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine kama TANAPA, Bandari na kwenye migodi.

No comments: