Migodi ya Dhahabu Nchini Kuanza Kulipa Ushuru - LEKULE

Breaking

26 Feb 2015

Migodi ya Dhahabu Nchini Kuanza Kulipa Ushuru

Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutangazia umma kuwa mgodi wa dhahabu wa Geita unaomilikiwa na kampuni ya AngloGold Ashanti; na migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara inayomilikiwa na kampuni ya Acacia Mining, imeanza kulipa ushuru wa huduma kwa kiwango cha asilimia 0.3 (0.3%) ya mapato ghafi kwa Halmashauri husika.

Halmashauri zitakazonufaika na malipo hayo ni: Mji wa Geita; Wilaya ya Geita; Mji wa Kahama; Wilaya ya Msalala; na Wilaya ya Tarime. Malipo hayo yanaanza tarehe 1 Julai, 2014.

Malipo hayo yanafuatia makubaliano kati ya Serikali na Kampuni zinazomiliki migodi husika kufanya marekebisho kwenye Mikataba ya Maendeleo ya Uchimbaji Madini (Mining Development Agreement - MDA) baina ya Serikali na Migodi ya Geita, Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara kuhusu ulipaji wa ushuru wa 0.3% ya uzalishaji kulingana na Sheria ya Local Government Finance Act, Cap.290 Revised Editions of 2002 badala ya Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka zilizokuwa zikilipwa awali.

Mha. Ngosi C.X. Mwihava
KAIMU KATIBU MKUU

No comments: