Kamanda Siro Atoa Ushahidi wake Katika Kesi ya Maandamano ya Mbunge Halima Mdee na Wenzake - LEKULE

Breaking

26 Feb 2015

Kamanda Siro Atoa Ushahidi wake Katika Kesi ya Maandamano ya Mbunge Halima Mdee na Wenzake

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeambiwa na Naibu Kamishna wa Polisi, Kamanda Simon Siro (54), ambaye amedai mahakamani kwamba alitoa zuio la kuandamana kwenda Ikulu kwa Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) kwa sababu maandamano hayo yangesababisha uvunjifu wa amani.

Alitoa madai hayo, wakati akitoa ushahidi dhidi ya Mbunge Halima Mdee na wenzake, kwamba baada ya kupitia vigezo vya kiusalama, njia waliyotaka kuitumia kufanya maandamano hayo inatumika na watu wengi hivyo nilishughulikia mara moja kuzuia maandamano hayo.

Kamanda Siro ambaye pia ni Mkuu wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  alitoa madai hayo wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka akisaidiana na Salum Mohamed Inspekta wa Polisi Jackson Chidunda.

Akiongozwa na Kweka, shahidi huyo alidai kuwa Oktoba 2, mwaka huu alipokea barua iliyopitia kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kutoka Bawacha wakiomba kufanya maandamani ya amani kwenda Ikulu.

“Katika barua hiyo Bawacha waliomba kufanya maandamano kwenda Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete kumtaka asipokee katiba inayopendekezwa… maandamano hayo yalipangwa kufanyika Oktoba 4, mwaka 2014 saa 3:00 asubuhi”alidai Kamanda Siro.

Akifafanua zaidi alidai kuwa "niwaagiza wafuasi wangu kwenda kukagua njia waliyotaka kuitumia lakini kwa bahati mbaya haikuwa salama kwa sababu ingeweza kusababisha  uvunjifu wa amani".

Alidai kuwa kwa nafasi yake anasimamia vikosi vyote vya kupambana na uhalifu kwa Kanda Maalum, kwa hiyo nilishughulikia mara moja kwa kuwajibu Bawacha kwamba maandamano hayo yasifanyike kwa sababu za vigezo vya kiusalama.

Aidha, Kamanda Siro aliomba mahakama ipokee nakala ya barua hiyo kama kielelezo lakini yalitokea mabishano ya kisheria na kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 3, mwaka huu ushahidi utakapoendelea kusikilizwa.

Mbali na Mdee, washtakiwa wengine ni,Rose Moshi , Renina Peter maarufu kama Lufyagila, Anna Linjewile, Mwanne Kassim, Sophia Fangel,  Edward Julius, Martha Mtiko na Beatu Mmari.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa hao wanadaiwa  Oktoba 4,mwaka 2014, katika mtaa wa Ufipa, bila kuwa na uhalali walikiuka amri halali ya kutawanyika iliyotolewa na Mrakibu wa Polisi Emmanuel Tille kwa niaba ya Jeshi la Polisi.

Pia wanadaiwa siku hiyo walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo moja la kutembea kwenda ofisi ya Rais Kikwete.

No comments: