Andrew Chenge AGOMA Tena Kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.....Aomba Aruhusiwe kukata Rufaa Mahakama kuu - LEKULE

Breaking

27 Feb 2015

Andrew Chenge AGOMA Tena Kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.....Aomba Aruhusiwe kukata Rufaa Mahakama kuu


MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ameendelea kupambana ili Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, lisiendelee kusikiliza shauri lake, licha ya pingamizi lake kutupiliwa mbali jana.
 
Chenge amewasilisha ombi la kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi wa baraza hilo, uliotolewa jana na kusomwa na Jaji Hamisi Msumi, ukisema madai yaliyowasilishwa kwenye pingamizi la mbunge huyo, hayalihusu baraza hivyo shauri linapaswa kuendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa.
 
“Tumeliangalia kwa makini pingamizi hili (la Chenge) na kuipitia amri ya Mahakama Kuu inayozuia suala la akaunti ya Escrow kujadiliwa na tumejiridhisha kuwa, Baraza hili halihusiani na orodha ya watu waliotajwa kwenye amri hiyo waliyowekewa pingamizi,” alisema Jaji Msumi.
 
Alisema baraza hilo limebaini katika amri hiyo, yako makundi yaliyotajwa kutojihusisha na suala hilo hadi pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi katika kesi ya msingi na katika makundi hayo, Baraza hilo la Maadili halikutajwa.
 
Alisema pia pingamizi kubwa, lililowekwa katika amri hiyo ni kuzuia kupelekwa bungeni na kujadiliwa kwa taarifa ya ukaguzi maalumu wa miamala ya Escrow na masuala ya umiliki wa IPTL.
 
“Hivyo basi, Baraza limeona hoja iliyowasilishwa na kukabidhiwa na mlalamikiwa haina msingi, hivyo imekataliwa,” alisema Jaji Msumi.
 
Chenge ang’ang’ana
Baada ya uamuzi huo, Chenge aliomba kuwasilisha hoja yake ya kukata rufaa akisema, “sina nia ya kubishana, ila nataka kuwasilisha nia ya kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huu wa Baraza ili suala hili litolewe uamuzi upya”.
Alisema anashangazwa na wanasheria wa baraza hilo, ambao hawajatumia muda wao ipasavyo kwa kwenda masjala ya Mahakama Kuu na kupitia amri hiyo ya Mahakama Kuu na kujiridhisha, kwa kuwa amri hiyo iko wazi, pana na imegusa maeneo mengi kuliko inavyofikiriwa.
 
“Naomba nitumie haki yangu ya kukata rufaa na kwenda Mahakama Kuu, naomba nipatiwe mwenendo mzima wa kesi, sasa sijui Baraza hili lina utaratibu wa kukata rufaa au mimi ndio nitalitambulisha suala hili kwa mara ya kwanza,” alihoji Chenge.
 
Kwa upande wake, Jaji Msumi alisema baraza hilo limemruhusu mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akate rufaa dhidi ya uamuzi wa baraza hilo Mahakama Kuu, jambo litakalosaidia pia kuweka historia ya kisheria.

 “Ni vyema tuachie Mahakama Kuu ambacho ni chombo cha juu kuliko Baraza hili, ili itueleze kama ni sahihi sisi kuendelea na shauri hili au la, kwa sasa sina uhakika kama kanuni zimetengwa kuhusu masuala ya rufaa kwenye Baraza hili,” alisema.
 
Alisema endapo Mahakama Kuu itaamua baraza hilo lisiendelee kusikiliza shauri hilo, shauri hilo halitasikilizwa, lakini ikiamuru liendelee, litaendelea kumhoji Chenge na kesi yake ya kukiuka maadili ya uongozi wa umma.
 
Juzi Chenge alisomewa rasmi mashitaka yanayomkabili na Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, ambayo ni pamoja na kutumia madaraka yake vibaya alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushauri Serikali iingie mkataba wa miaka 20 na kampuni ya IPTL.

 Aidha, anadaiwa baada ya kustaafu wadhifa huo wa uanasheria mkuu wa Serikali Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekezi wa kampuni wa VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa za asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL.
 
Lakini, pia mwanasheria huyo anadaiwa na baraza hilo, kuingia mkataba na kampuni ya VIP, uliompatia manufaa ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na fedha hizo ziliingizwa Februari 5, mwaka jana katika akaunti ya mlalamikiwa namba 00120102523901, iliyopo kwenye Benki ya Mkombozi Tawi la St Joseph jijini Dar es Salaam.
 
Baada ya kusomewa mashitaka hayo juzi, mbunge huyo alikataa kesi hiyo kusikilizwa na kuwasilisha pingamizi hilo la kutaka suala hilo kutoendelea kusikilizwa kwa kuwa tayari kuna kesi ya msingi Mahakama Kuu inayoendelea kusikilizwa.

No comments: