UN: Ugaidi hauna mfungamano na dini maalumu - LEKULE

Breaking

22 Jan 2015

UN: Ugaidi hauna mfungamano na dini maalumu



Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, ugaidi haufungamani na dini au madhehebu fulani na kusisitiza kwamba viongozi wote wa dini ulimwenguni wanalaani na wanapinga kwa nguvu zao zote vitendo vya kigaidi na vya kufurutu mipaka. Farhan Haq, Msemaji wa Ban Ki moon ameelezea nafasi ya viongozi wa kidini katika kuzuia kusambaa na kuongezeka makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka na ya kigaidi yanayojinasibisha na dini ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, ugaidi kamwe haufungamani na dini maalumu na kwamba wafuasi wa makundi yenye kufurutu mipaka kutoka dini yoyote ile wanaweza kutekeleza vitendo vya kigaidi. Farhan Haq amebainisha kuwa, walimwengu wanapaswa kuelewa kwamba vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na baadhi ya wafuasi wa dini fulani, havimaanisihi kwamba dini hiyo inahubiri na kuwashajiisha wafuasi wake kutekeleza vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hadi sasa umoja huo umefanya mazungumzo na viongozi wengi wa kidini duniani na kusisitiza kwamba viongozi hao wote wamelaani vikali ugaidi unaofanywa kwa namna yoyote ile. Farhan Haq ameeleza kwamba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa daima amekuwa akiwataka wafuasi wa dini mbalimbali kuwavumilia wafuasi wa dini nyingine ili kupatikane amani na utulivu duniani.

No comments: