Wagombea nafasi ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wameshauriwa
kupima afya zao kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho, ili
kuepuka gharama za matibabu ya mara kwa mara za kiongozi huyo mkubwa wa
nchi.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la
Katiba, Deus Kibamba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini
Dar es Salaam leo, ambapo pamoja na wagombea urais alipendekeza pia na
wagombea wenza kupima afya zao na majibu yao kuwa wazi ili kuepuka
gharama zisizo za lazima.
Kibamba alisema alichojifunza kwenye Uchaguzi Mkuu
wa Zambia baada ya marais wawili kufariki wakiwa Ikulu na kusababisha
nchi kuingia kwenye gharama za kuchagua marais mara mbili kwa kipindi
cha miaka sita, kitu kilichowapa mtizamo mpya ambao ni kupima afya za
wagombea urais kabla ya kuingia Ikulu.
“Suala la viongozi kupima afya hapa nchini
limekuwa ni siri sana, lakini kwa mfano huu, hakuna budi viongozi kupima
na kubainisha majibu ya afya zao ili kuangalia kama wanaweza kumudu
mikikimikiki ya urais bila kuitia nchi gharama ya kuwatibia kila mara
tena kwenye hospitali za nje, ”alisema Kibamba.
Nae Mjumbe wa Jukwaa la katiba, Islael Ilunde
alisema kuwa wanaangalia uwezekanao wa kuitisha midahalo kwa wagombea
ili kuwapa nafasi wananchi ya kusikia kile kinachotakiwa kufanywa na
wagombea hao mara baada ya kushinda nafasi wanazozigombea.
Alisema siyo lazima kufanya mdahalo wa wagombea wa
nafasi za juu , bali hata wanaogombea nafasi za kawaida wapiga kura wao
wanatakiwa wafahamu kwa undani uwezo wao wa kujieleza na kupambanua
mambo na ahadi zao.
“Kama vyombo vya habari na wadau wengine
watashindwa kuanzisha midahalo ya kuwahoji viongozi, sisi tutazungumza
na wadau wetu kuona ni kwa namna gani tutalifanya jambo hilo muhimu kwa
kipindi hiki, ”alisema Ilunde.
No comments:
Post a Comment