Kutoka Bungeni: Muswada wa Takwimu wadunda tena bungeni, warudishwa - LEKULE

Breaking

27 Jan 2015

Kutoka Bungeni: Muswada wa Takwimu wadunda tena bungeni, warudishwa



Muswada wa Sheria ya Takwimu uliokuwa uwasilishwe bungeni katika mkutano wa 18, hautawasilishwa tena hadi hapo taratibu za kikatiba zitakapokamilika. 
Taarifa ya kutowasishwa kwa muswaada huo bila kutaja sababu zilitolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, muda mfupi kabla ya kuahirisha kikao cha leo.
“Muswada wa Takwimu unaondoka kwasababu bado serikali inataka kuufanyia kazi,”alisema Spika Makinda.
Akizungumza nje ya bunge, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema kuwa muswada umeondolewa ili kuwezesha kufuata taratibu za kikatiba.
“Inabidi muswada huu uende Zanzibar kujadiliwa na upate theluthi mbili wakati wa kupigiwa kura bungeni kutoka kwa wabunge wa pande zote,”alisema Nchemba.
Hii ni mara ya pili kwa muswada huo kushindwa kupitishwa baada ya kukosekana kwa theluthi mbili ya wabunge bungeni.
Aidha, Spika Makinda alisema muswada wa Sheria ya Utawala wa Kodi uliokuwa upigiwe kura leo, utapigiwa kura kesho baada ya kukosekana kwa theluthi mbili ya wabunge kutoka pande zote.
“Muswada wa Utawala wa Kodi bado kuna kazi ndogo tu ya kupigiwa kura lakini tumetambua bado wabunge wote hawajafika,”alisema Makinda.
Alizitaka kamati za vyama kukutana ili kuweza kupata utaratibu mzuri wa kuifanya kazi hiyo kesho.
Katika hatua nyingine, Spika Makinda alitangaza kuchaguliwa kwa Mbunge wa Bukoba Vijijini, (CCM) Jasson Rweikiza, kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Nafasi hiyo iliachwa wazi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja baada ya Bunge kutaka kuvuliwa kwa nafasi hiyo baada ya kupata mgawo katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow

No comments: