SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limefanikiwa kulikomboa basi la timu ya soka la wanaume ya Tanzania, ‘Taifa Stars,’ huku likikiri kupata usumbufu mkubwa wa deni la kurithi la shilingi mil. 140 lililosababisha kukamatwa kwa chombo hicho ghali.
Basi kubwa la Taifa Stars aina ya Yutong lililotolewa na wadhamini wa Taifa Stars, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji cha Kilimanjaro Premium Lager, lilikamatwa katikati ya mwaka jana kwa agizo la Mahakama, ambapo TFF ilitanguliza sh. Mil 70.
Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, amesema harakati mbalimbali za ndani na nje ya Mahakama, zimefanikisha kukombolewa kwa basi hilo na sasa liko mikononi mwao tayari.
“Hili ni suala la kisera na lilipaswa kuzungumzwa na Rais wa TFF, lakini kifupi ni kwamba tumemaliza kulipa deni husika ambalo TFF yetu ilirithi kutoka kwa TFF iliyopita, hivyo tumelikomboa rasmi basi hilo na liko mikononi mwetu,” Amesema Mwesigwa.
Mwesigwa amesema kuwa, kimsingi deni hilo liliwapa wakati mgumu na hawakuwa na njia ya kutolilipa baada ya kulirithi na kwamba liliwaumbua vya kutosha, ingawa wanashukuru kwa jitihada zao za kulikomboa kuzaa matunda.
No comments:
Post a Comment