ANAFAHAMIKA sana visiwani hapa kwa jina la JANJA. Huyu si mwingine, bali ni Amour Omary, mfungaji wa bao pekee la mechi kali ya robo-fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu ya Yanga na JKU kwenye Uwanja wa Amaan Januari 8.
Ikiwa inapumlia mashine kutokana na uimara wa kikosi cha Yanga kilichokuwa kikicheza nusu uwanja, JKU ilifanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa wanajangwani dakika ya 72, beki wa pembeni Oscar Joshua alipozubaa na kumpa nafasi kiduchu ya kupiga shuti mshambuliaji huyo.
Pengine kutokana na kutomjua vizuri, lakini Yanga ilipaswa kujua kwamba Janja ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Zanzibar msimu huu akiwa ametupia mara nane pia msimu huu na kuongoza safu ya wafumania nyavu hatari wa ligi hiyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm na msaidizi wake Boniface Mkwasa hawakukosa hata mechi moja kwenye Uwanja wa Amaan kabla ya mechi hiyo, kila mechi walionekana Jukwaa la VIP wakisoma mbinu za wapinzani. Hakika walipaswa kumjua mkali huyu wa mabao!
Kabla ya mechi hiyo, Janja alikuwa amefunga mabao mawili magumu na maridhawa, moja dhidi ya Mafunzo waliposhinda 2-0 katika mechi yao ya Kundi C na jingine katika mechi yao ngumu ya mwisho ya Kundi C dhidi ya Mtibwa Sugar iliyomalizika kwa sare ya 1-1.
Kosa la Joshua kuukimbia mpira akitaka aubutue kwa mguu badala ya kuupiga kichwa, likaigharimu Yanga iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutinga fainali mbele ya Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliyekuwa mgeni rasmi.
jANJA
Janja (kulia) akiongea na mchezaji wa Simba sc, Awadh Juma
Janja alimkimbilia kocha wake, Malale Hamsin Keya na kumkumbatia huku akilia kwa furaha. Hakika halikuwa kosa kulia kutikana na furaha ya kufunga bao lililoing’oa timu ngumu ya Yanga iliyokuwa na nyota watano wa kigeni akiwamo mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita, Mrundi Amisi Tambwe.
“Nimekuwa mchezaji kwa muda mrefu sasa, kazi yangu ni kufunga. Yanga walitubana sana lakini kama mshambuliaji nilituliza akili vilivyo kabla ya kupiga shuti lile.
“Ilikuwa nafasi nzuri kwetu baada ya Yanga kujisahau kidogo kutokana na kutushambulia muda wote. Kujituma mazoezini na kuzingatia maelekezo ya mwalimu wangu (Malale) ndiyo siri ya mafanikio yangu,” alisema Janja katika mahoajino maalum na NIPASHE iliyotinga nyumbani kwake maeneo ya Shaurimoyo visiwani hapa mwishoni mwa wiki.
AWEKA REKODI KIBAO
Mabao yake matatu aliyoyafunga, si kwamba yameishia kuwakamata William Wadri (KCCA), Andrey Coutinho (Yanga) na Ibrahim Hajibu (Simba) wenye mabao matatu pia, bali yamemfanya kuwa mshambuliaji bora zaidi katika michuano hiyo licha ya kuzidiwa bao moja na kiungo Simon Msuva wa Yanga.
Kwanza, ni mchezaji pekee aliyefunga mabao matatu katika mechi tatu tofauti dhidi ya Mafunzo, Mtibwa Sugar na Yanga. Janja ni mchezaji wa pekee aliyeifunga Yanga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka, timu hiyo ya Jangwani ikifunga mabao tisa.
Ni mchezaji pekee aliyemfunga kipa Ali Mustafa ‘Barthez’ wa Yanga katika michuano hiyo kipa huyo akidaka mechi tatu kati ya nne. Kipa Doe Munishi ‘Dida’ alidaka mechi yao ya mwishi ya Kundi A waliyoshinda 1-0 dhidi ya Shaba C.
Nne, Janja ni mchezaji pekee aliyefunga bao katika dakika ya 72 (amefunga mabao mawili dhidi ya Mafunzo na Mtibwa Sugar katika dakika hiyo). Mabao mengine 35 (kabla ya mechi za nusu-fainali) yalifunga dakika za 7, 9, 11, 13, 18, 20, 21 (mawili), 27 (mawili), 33, 34, 36, 38, 40, 44, 46, 47, 48, 49, 53, 54, 56, 62, 64, 65, 67, 75, 76, 80 (mawili), 82, 84, 86, 89 na 90′.
Mechi nyingine tatu za robo fainali zilimalizika kwa suluhu, sare ya bao moja na kipigo kikubwa cha 4-0 lakini goli lake dhidi ya Yanga likafanya matokeo tofuati ya robo fainali. Simba walishinda 4-0 dhidi ya Taifa ya Jang’ombe, Mtibwa walitoka 1-1 dhidi ya Azam FC kabla ya kushinda kwa penalti 7-6 wakati Polisi walitoka suluhu dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi KCCA ya Uganda kabla ya timu hiyo ya Zanzibar kufuzu kwa matuta 5-4.
Sita, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema mwishoni mwa wiki kwamba bao la Janja dhidi ya Yanga ndiyo bora katika mashindano hayo mwaka huu (kabla ya mechi za nusu fainali).
“Ni mshambuliaji anayejua kufunga, amaefunga mabao mazuri ambayo huchoki kuyatazama hata katika video. Goli alilowafunga Yanga, ninafikiri ndiyo goli bora la mashindano haya kwa sasa.
Tutaendelea kusajili wachezaji wa Zanzibar katika kikosi chetu kwa sababu hapa kuna vipaji. Wakati mimi ninacheza Mtibwa, tulikuwa na nyota wengi tu kutoka Zanzibar akiwamo Abdi Kassim,” alisema Mexime.
Saba, Janja ndiye amefunga bao la mapema zaidi katika michuano hiyo mwaka huu. Pia ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mashindano hayo mwaka huu (kabla ya mechi za nusu-fainali). Alifunga bao hilo dakika ya saba katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C dhidi ya Mafunzo FC kwenye Uwanja wa Amaan Mwaka Mpya.
Tisa, mabao yake yote matatu (kabla ya mechi za nusu-fainali) yana uhusiano wa namba saba (7). Kama ilivyodokezwa hapo juu bao la kwanza alilifunga dakika ya ya saba na magoli mengine mawili ameyafunga dakika ya 72, hivyo kuoneakana kama ana nyota ya Na. 7 ambayo ndiyo tarehe yake ya kuzaliwa kwani mkali huyo ya kucheka na nyavu alizaliwa Saba-Saba 1985. Na. 7 pia ni namba ya jezi ya Cristian Ronaldo ambaye ndiye mchezaji anayemkubali duniani.
Rekodi ya 10 iliyowekwa na Janja ni kufunga mabao mawili, yote akipiga mashuti nje ya boksi la wapinzani wao. Bao lake dhidi ya Mtibwa Sugar alilifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa faulo iliyopenyezwa ndani ya sita. Hakuna mchezaji mwingine aliyefunga mabao mawili nje ya boksi.
ALIKOTOKA KISOKA
Janja anasema alianza kucheza soka akiwa na timu ya Gulioni visiwani hapa akifundishwa na kocha Yusuph Chunda (sasa Kocha Mkuu wa Shangani FC ya Zanzibar pia) kabla ya kujiunga na Mlandege 2003/4 na kuitumikia kwa misimu miwili kabla ya kutimkia Miembeni, zote za visiwani hapa.
“Nikiwa Miembeni kwa misimu mwili sikung’ara sana kwa sababu sikupewa nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na uwapo wa wakali wengine zaidi yangu kina (Amri) Kiemba na wenzake wa wakati huo, Nilikuwa ninachezeshwa dakika tano zikizidi sana dakika 10,” Janja anasema.
“Nikaenda Oljoro JKT ya Arusha tukafanikiwa kuipandisha VPL na mimi nilikuwa mfungaji bora wa timu lakini kukatokea migogoro mimi na wenzangu kina (Nassoro Masoud) Chollo, Juma Mohamed na Ally Hamza tukalazimika kuikimbia.
“Baada ya kutoka Arusha, nikajiunga na Mtende (iliyokuwa Kundi B la Kombe la Mapinduzi mwaka huu) nikaichezea kwa misimu miwili kabla ya kujiungan na Bandari lakini timu hiyo ilivunjwa nikaamua kurudi Miembeni nikawa mfungaji bora nikifunga mabao 15 huku tukimaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar kabla sijajiunga na JKU msimu uliopita,” anasema zaidi Janja.
Licha ya kucheza katika timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa, Janja anaweka wazi kwamba yeye si askari na kwamba tayari klabu za Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zimeanza kutuma watu kwake kufabnya mazungumzo ya kumsajili msimu ujao.
MAISHA BINAFSI
Janja anayekocha na ‘VITU’ vya mchezaji bora wa dunia mara mbili, mshambuliaji wa Real Madrid ya Ligi Kuu ya Hispania, Ronaldo, anasema kuwa ana mke (Savina Nyasa) na wamebahatika kupata mtoto mmoja (Mohamed Amour).
Mchezaji huyo anayependa kula wali/maharage, ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto sita (watatu wa kiume) ya Bw. Omary Janja na Bi. Rose Musele.
Mbali na kumkubali Ronaldo, Janja anasema: “Upande wa wachezaji wa Tanzania, ninamkubali sana (Haruna Moshi) ‘Boban’. Unajua ukiacha vitendio ambavyo amekuwa akiwakera baadhi ya watu, Boban ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.”
“Nilishawishika kucheza mipira baada ya kuvutiwa na kaka yangu, Eg Mohamed ambaye alikuwa akichezea KMKM miaka ya ’96, ’97,” anasema zaidi Janja. ambaye anaamini muda si mrefu ataitwa katika kikosi cha Taifa Stars kutokana na uwapo wa Nooij katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu.
Makala hii imeandikwa na Sanula Athanas, Mwandishi Mwandamizi wa gazeti la NIPASHE.
No comments:
Post a Comment