Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wanakutana hii leo kwa mkutano wa kwanza chini ya usimamizi wa katibu mkuu mpya wa NATO Jens Stoltenberg
Akizungumza hapo jana, Katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema ni wakati muafaka wa kukutana ambapo Ukraine inashuhudia uchokozi kutoka Urusi na Ulaya ikijikuta katika kitisho kutoka kwa kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa dola la kiislamu IS.
Rais wa Afghanistan na mtendaji mkuu-cheo ambacho ni sawa na waziri mkuu,Abdullah Abdullah pia watahudhiria mkutano huo unaofanyika mjini Brussels,Ubelgiji kwa mazungumzo kuhusu kipindi cha mpito cha kuondoka kwa wanajeshi wa NATO nchini Afghanistan na kutolewa mafunzo kwa wanajeshi wa Afghanistan mwishoni mwa mwaka huu.
Kikosi cha dharura kuundwa
Mawaziri hao watazindua rasmi tume ya kijeshi ya kutoa mafunzo na ushauri kwa jeshi la Afghanistan ambayo itaanza kazi tarehe mosi mwezi Januari ili kukabidhi jukumu la ulinzi wa jeshi la Afghanistan.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani na mawaziri wenzake watashughulikia ajenda kuu ya kuhakisha kuundwa kwa kikosi maalum kitakachoweza kukabiliana na vitisho visivyotabirika ambavyo jumuiya hiyo ya NATO itakumbana navyo.
Katika mkutano wa mwezi Septemba, viongozi wa nchi 28 wanachama wa NATO walikubali hivi sasa wanakabiliwa na mizozo iliyo tofauti na waliyoizoea katika kipindi cha nyuma kisiasa na kivita ambayo inahitaji mfumo mpya wa kijeshi kukabiliana nayo.
Viongozi hao walikubaliana kuundwa kwa kikosi maalum kitakachokuwa na wanajeshi 4,000 ifikapo mwaka 2016 lakini hii leo wanatarajiwa hata kuharakisha kuundwa kwa kikosi hicho ili kianze kuhudumu ifikapo mwaka ujao huku Ujerumani na Uholanzi zikiwa tayari kuchangia pakubwa katika kikosi hicho.
Mawaziri hao pia watatathimini juhudi za kuzihakikishia nchi za Baltiki na Poland,Romania na Bulgaria kuwa ulinzi utaimarisha katika kanda hiyo ili kuzuia uwezekano wa uchokozi kutoka Urusi.
Ukraine kusaidiwa kijeshi na NATO
Kuhusu suala la Ukraine,mawaziri hao wa mambo ya nje wanatarajiwa kuidhinisha hazina nne za kufadhili shughuli za kijeshi kuisaidia serikali ya Ukraine kupamabana na waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanaotaka kujitenga kwa eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Magari ya kijeshi yakiingia mashariki mwa Ukraine
Magari ya kijeshi yakiingia mashariki mwa Ukraine
Stoltenberg ameitaka Urusi kupunguza shughuli zake za kijeshi katika mpaka kati ya nchi hiyo na Ukraine. Suala la iwapo Ukraine inaweza kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO halitakuwa katika ajenda.
Wengi wa mawaziri hao watarejea katika makao makuu ya NATO mjini Brussels hapo kesho kwa mkutano utakaoongozwa na Kerry kujadili kampeini ya kivita ya Marekani na washirika wake dhidi ya IS nchini Syria na Iraq.
NATO imesema iko tayari kuisaidia Iraq iwapo iatomba msaada wa kijeshi lakini Stoltenberg amesisitiza jumuiya hiyo ya kujihami haitashiriki moja kwa moja katika mzozo huo.
No comments:
Post a Comment