Mwanafunzi aliyefunika hisabati darasa la 7 - LEKULE

Breaking

10 Nov 2014

Mwanafunzi aliyefunika hisabati darasa la 7


Mwanafunzi bora wa somo la Hisabati katika mitihani ya taifa ya darasa la saba iliyofanyika nchini Septemba mwaka huu, Rachel Kiunsi (13), ameeleza siri ya mafanikio yake kuwa ni kujituma katika masomo na kuwaheshimu walimu.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana kutoka mkoani Singida, Rachel ambaye alikuwa anasoma shule ya msingi Kimara 'B', jijini Dar es Salaam, alisema alikuwa na bidii ya kujituma katika masomo yake hasa katika la hisabati na   ya Sayansi na kwamba alikuwa anashindwa kupata usingizi bila kujisomea usiku.

Akizungumzia jinsi alivyopokea taarifa za matokeo yake, Rachel alisema ni kwa furaha na alikuwa akitengemea kufaulu, lakini siyo kwa mafanikio kama hayo aliyoyapata. 
“Nanamshukuru sana Mungu  kwani nilikuwa namwomba atende maajabu katika matokeo yangu... nilikuwa nasali kila nikifanya mtihani na kumaliza,” alisema Rachel, ambaye alikuwa akiishi na bibi yake Kimara.

Aliwashukuru walimu wake wa masomo yote kwa juhudi za kuwafundisha vizuri wanafunzi wote katika shule hiyo kwani walikuwa wakiingia darasani kwa muda wa ziada na kutoka saa 11 jioni.

“Mimi nawashauri wanafunzi wenzangu tuliomaliza wote na kufaulu kuwa tuongeze bidii katika masomo yetu ya Sekondari kwani bila juhudi hatutaweza kufaulu kama tulivyofaulu sasa,” alisema.

Akielezea masomo anayoyapenda, Rachel,  alisema kuwa ni  ya Sayansi na ndoto zake zilikuwa ni kusoma katika shule ya sekondari ya vipaji maalumu ya wasichana ya Kilakala iliyopo mkoani Morogoro.

MAMA MZAZI AZUNGUMZA
Kwa upande wake, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Grace Kiunsi, akizungumza na NIPASHE kwa simu kutoka Singida, alisema matokeo ya mtoto wake aliyapata kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) na alifurahi, lakini hakufahamu kama ameongoza katika somo la Hisabati.

“Kusema ukweli nilipata furaha ya hali ya juu baada ya kuona matokeo ya mwanangu kuwa amefaulu kwa daraja la kwanza ‘A’, kwa masomo yote nilimpigia simu baba yake ambaye yupo masomoni katika Chuo cha Biblia Dodoma na kumweleza naye alifurahi sana,” alisema Kiunsi.

Alisema taarifa za kuwa mwanaye ameibuka kinara wa hisabati nchi nzima alizipata kupitia gazeti la NIPASHE ndipo furaha yake ilipozidi kwani hakufaulu kwa daraja la kwanza tu bali hata kitaifa.

Aliongeza kuwa mwanaye hakuna kitu anachopenda zaidi ya kusoma kwani kuna wakati mwingine alikuwa anashindwa kula au kulala kama hajamaliza kazi alizopewa na walimu wake shuleni.

“Rachel alikuwa ni mwenye heshima sana kwa walimu wake ilifika kipindi hata wazazi wake alikuwa hatutii kama anavyowatii walimu wake,” alisema Kiunsi.
Alisema hiyo ndiyo siri ya mafanikio ya mwanaye katika masomo yake, hivyo aliwaomba walimu wa shule aliyosoma Rachel kuongeza bidii kwani ndiyo zitakazoinua shule yao.

MWALIMU MKUU ASIMULIA
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Zuxine Mponda, alisema Rachel alikuwa ni mtoto wa kipekee katika shule yake kwani alikuwa ni mtiifu, msafi, mpole na msikivu kwa walimu wake.

Alisema walimu walikuwa wanategemea matokeo mazuri kwa wanafunzi wao kwani shule yake ina misingi mizuri ya kuaandaa wanafunzi kufaulu mitihani yote sio tu ya mwisho.

Alisema  mwanafunzi huyo alikuwa akiongoza katika mitihani ya majaribio (moku), ya wilaya na mkoa na wastani aliokuwa akiupata ni wa 50 kwa 50 hasa katika Hisabati.

Mwalimu Mponda, alisema kuwa katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa darasa la saba mwaka 2012 shule yake ilishika nafasi ya tatu kiwilaya na wanafunzi watatu walishinda kwenda katika shule ya Sekondari vipaji ya wanaume ya Ilboru. 

Alisema wanafunzi waliomaliza darasa la saba katika shule yake mwaka huu ni 191 huku wasichana wakiwa 90 na wavulana  101.

Mpanda alisema wanafunzi waliopata alama ‘A’ katika somo la hisabati ni 37, Kingereza 13, Sayansi 12, Maarifa 16 na Kiswahili 16.

Aliongeza kuwa kutokana na ufaulu huo matokeo ya shule yake ni mazuri kwani wanafunzi waliopata daraja la kwanza ‘A’ katika masomo yote walikuwa watatu huku ‘A’ zikiwa ni 13 ‘B’ 76, ‘C’ 84, ‘D’ 18 huku hakuna mwanafunzi aliyepata alama ya F au E. 

Aliongeza kuwa utamaduni wa shule hiyo kwa mwanafunzi yoyote aliyefanya vizuri ni kupewa zawadi hivyo wakapofanya kikao cha kamati ya shule watachagua zawadi ya kumpa mwanafuzi huyo.

Aliitaka Serikali kubadilisha utaratibu wa kulinganisha wastani kwa shule za Serikali na shule binafsi ili kumpata mwanafunzi bora au shule bora kwani mazingira ya ufundishaji ni tofauti .

MWALIMU WAKE AMWELEZEA
Naye mwalimu wa Hisabati shuleni hapo, Aron Mwinyi, alieleza siri ya mafanikio ya ufaulu huo kwa wanafunzi wake kwa kusema waliandaliwa vyema.

Alieleza kuwa shule hiyo ina utaratibu wa kuwaandaa wanafunzi toka awali na kuwajengea ukaribu ili wanapokuwa na tatizo masomo iwe rahisi kutatuliwa.

Alielezea sifa za Rachel na kusema kuwa alikuwa ni mwanafunzi makini tangu darasa la tano kwani alikuwa akiwasumbua walimu pale anapokuwa hajaelewa na hiyo ikamjengea uwezo wa kuongoza darasani katika kila somo. 

“Katika shule yetu hapa hakuna tabia ya wanafunzi kujitenga kwa kujiona kuwa wanaakili sana, hapa wanafunzi wote ni sawa na wanafundishana na hiyo ndio sababu kuu ya ushindi huu kwa shule yetu,” alisema Mwinyi.

Mwinyi aliongeza kuwa walimu wanashirikiana katika ufundishaji kwani wakati mwanafunzi anakuwa na shida na mwalimu wake wa somo hayupo, mwanafunzi akimwona mwalimu yeyote anamsaidia.

Kwa upande wa mwalimu wa Kingereza, Privatus Mbehoma, alisema ni faraja kwa wanafunzi wao kufaulu masomo ya Kingereza na maarifa kwani ni masomo ambayo ufaulu wake ni mdogo lakini kwa shule yake wamefaulu kwa kiwango cha kuridhisha.

Juzi Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alitangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba uliofanyika Septemba mwaka huu huku wavulana wakiwa wameongoza na kanda ya ziwa ikitoa shule nane katika 10 bora.

Matokeo hayo yalionyesha kuwa watahimiwa wengi hawakufanya vizuri somo la Hisabati lenye ufaulu wa asilimia 37.56 huku somo la Kiswahili ufaulu wake ukiwa unaongoza kwa asilimia 69.70.

Katika Somo la Hisabati kati ya watahimiwa 34 waliopata 50 kwa 50 wasichana ni nane na wavulana ni 26.

UPINZANI WAKOSOA MATOKEO
Waziri kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lymo (Chadema), amesema ongezeko la ufaulu wa darasa la saba mwaka huu haufanani na halisi inayoonekana kwenye sekta ya elimu nchini.

Taarifa ya Necta) ilisema ufaulu umeongezeka kwa asilimia 6.38 ikilinganishwa na mwaka jana.

Lyimo alisema ili kutokea kiwango hicho cha ufaulu, sekta ya elimu ingeonekana kuwa na mabadiliko ya dhahiri tofauti na sasa ambapo kinachoshuhudiwa ni matamko, kama vile Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Lymo ambaye kitaaluma ni mwalimu, alisema pamoja na hali hiyo, ufaulu hafifu unaoendelea kuonekana kwenye somo la Hisabati ni kiashiria
kikuu cha uwezo duni wa wahitimu.

Alisema mwanafunzi yeyote anayefaulu somo hilo anakuwa na uwezo mkubwa kitaaluma na kwamba akiamua kujifunza somo lolote anaweza kulimudu.

Alisema ufaulu ndogo kiini chake kikuu ni serikali kutowekeza katika sekta ya ajira, kwa lengo la kupata matokeo mazuri yaliyo ya kweli.

“Na ukienda mbali zaidi utabaini kuwa wengi wa wanaofaulu ni watoto wa wenye kipato cha juu na kati, wanaomudu kusomesha watoto wao kwenye shule binafsi, upo uwezekano mkubwa wa watoto wengi wa maskini kubaki bila elimu,” alieleza.

Lymo alisema hakushangazwa na kauli ya Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, iliyotaka wananchi watarajie matokeo mazuri zaidi katika matokeo ya kidato cha nne na kwamba hata hayo yatakuwa matokeo mazuri kwa wingi siyo kwa ubora.

HAKI ELIMU
Meneja wa Idara ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Taasisi ya Haki Elimu, Godfrey Boniventura, alisema  katika miaka ya nyuma kiwango cha ufaulu kiliikuwa kinafika asilimia 80 hadi 85 tofauti na sasa wanafunzi wanapata matokeo yasiyoridhisha..

Alisema matokeo mabaya ya somo la Hisabati yamesababishwa na namna ya somo linavyofundishwa bila kuzingatia mbinu zinazofaa, kukosekana kwa mfumo madhubuti wa tathmini ya ufundishaji na ukaguzi huku akiitaka serikali kubadili mfumo wa ukaguzi kwenye shule.

No comments: