Kaya masikini 40,218 Singida zanufaika na pesa za TASAF - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 22 February 2016

Kaya masikini 40,218 Singida zanufaika na pesa za TASAF


TASAF Singida
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Singida umetoa msaada zaidi ya shilingi 11.2 bilioni kwa ajili ya kunusuru kaya masikini 40,218 kati ya Septemba 2014 na Desemba mwaka jana.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni na Mbunge Viti Maalum, Fatma Toufiq, wakati akifungua kikao cha siku moja cha kuwajengea uwezo  waratibu, madiwani na wadau wengine wa  mpango wa TASAF III, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Fatma Toufiq
Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Fatma Toufiq, akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waratibu wa TASAF halmashauri mpya ya Itigi. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Singida, Boniface Temba na wa kwanza kushoto, ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Itigi.
Alisema kaya hizo maskini zilizonufaika na msaada huo,zipo kwenye Vijiji 2,726 na kati ya Vijiji hivyo, Vijiji 30 ni vya Halmashauri ya Itigi ambayo ina Vijiji 39.
Akifafanua, Fatma alisema wilaya ya Ikungi imepewa zaidi ya shilingi Bilioni Tatu, Iramba 1.9 bilioni, wilaya ya Singida Bilioni 2, Manispaa ya Singida Bilioni moja na Ofisi ya katibu tawala mkoa milioni 104.5.
Mkuu huyo wa wilaya,alisema lengo la msaada huo, ni kuzijengea uwezo na kuziwezesha kaya hizo  maskini kuongeza kipato, ili ziweze kumudu kugharamia mahitaji yao muhimu na masomo ya watoto wao.
Patrick Kasango
Mratibu TASAF mkoa wa Singida, Patrick Kasango, akitoa nasaha zake kwenye ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waratibu wa TASAF wa halmashauri mpya ya Itigi wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Katika hatua nyingine, DC huyo alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na msaada huo, ni kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na pia ongezeko la wanafunzi walioandikishwa mwaka jana.
“Pia msaada huo, umepunguza vifo vya akina mama wajawazito na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 kwa mwaka jana. Vifo hivyo vimepungua ikilinganishwa na mwaka juzi, kutokana na akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ikiwa ni sharti mojawapo la mpango huo,” alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya, amewataka viongozi wa watendaji kuendelea kuwashauri na kuwahamasisha wazitumie fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuleta matokeo chanya na kuondoka kwenye umaskini.
Majuto Kawambwa
Mratibu wa TASAF halmashauri ya wilaya ya Ikungi na manispaa ya Singida, Majuto Kawambwa, akitoa mada yake iliyohusu majukumu ya waratibu wa TASAF ngazi ya halmashauri na wadau wengine wa mfuko huo,juzi kwenye semina ya siku moja iliyohudhuriwa na wadau TASAF halmashauri wilaya Itigi.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF mkoa wa Singida,Patrick Kasango, alisema watendaji wa vijiji na kata hawaruhusiwi kujihusisha na shughuli ya ulipaji wa  fedha za TASAF kwa walengwa.
“Katika mpango huu wa TASAF III, watendaji wamepewa jukumu la kusimamia tu zoezi la utoaji wa msaada wa fedha za kunusuru kaya maskini, na si vinginevyo. Aidha, hairuhusiwi fedha za walengwa kuchukuliwa na mtu mwingine, mlengwa asiohudhuria siku ya kutoa msaada, fedha zake zitarudishwa na zitalipwa awamu itakayofuata,” alifafanua Kasango.
Fatma Toufiq
Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida na mbunge viti maalumu Dodoma, Fatma Toufiq (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wataribu wa TASAF mkoa na halmashauri wilaya ya Itigi.Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Itigi, Msafiri Abdalah na anayefuatia ni Mwenyekiti wa halmashauri Itigi, Alli Minja.
Post a Comment