Bosi mpya NMG: Nitasimamia weledi na uhuru wa habari - LEKULE

Breaking

30 Jul 2015

Bosi mpya NMG: Nitasimamia weledi na uhuru wa habari

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nation Media Group (NMG), Joe Muganda akizungumza na mwakilishi Mkazi wa Aga Khan Development Network (AKDN), Amin Kurji (Kulia) , pamoja na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Hanif Jaffer na  mwenyekiti wa Bodi ya MCL Leonard Mususa( wa pili kushoto), wakati wa hafla ya kumkaribisha iliyofanyika kwenye Hotel ya Serena, jijini  Dar es Salaam juzi. Picha na Emmanuel Herman


Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu mpya wa kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG), Joe Muganda ameahidi kusimamia kikamilifu weledi na uhuru wa vyombo vya habari vya kampuni hiyo, ambavyo ni pamoja na magazeti ya The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti yanayozalishwa na Mwananchi Communication Limited.

Muganda alisema hayo wakati akitambulishwa kwa wafanyakazi wa Mwananchi Communications Limited na wadau wa habari. Mwananchi Communication Limited ya Tanzania na The Monitor ya Uganda ni kampuni tanzu za NMG.

Muganda, aliyeanza kazi na NMG takriban mwezi mmoja uliopita akichukua nafasi ya Linus Gitahi, alisema kwa kipindi chote cha mkataba wake anapenda kuongoza kampuni ambayo habari zake zinaaminika na kila mtu na kufanya kazi kwa uhuru wa hali ya juu.
Muganda aliwaeleza wadau waliohudhuria hafla ya utambulisho huo jijini hapa juzi kuwa wakati huu wa uchaguzi, MCL haitafungamana na upande wowote na itaendelea kutoa habari kwa uwajibikaji mkubwa.

“Uwajibikaji ni jambo la msingi sana unapoongoza chombo cha habari kwa sababu iwapo ukikosea kidogo unaweza kulipeleka taifa katika uelekeo mbaya,” alisema Muganda.
“Lazima tuhakikishe habari ni ya kweli, inatenda haki kwa wote na kubwa zaidi ni kuwa huru… hiyo misingi ndiyo nitakayoisimamia kikamilifu,” alisema Muganda.

Ahadi hiyo aliirudia tena jana asubuhi wakati akitambulishwa kwa wa wafanyakazi wa MCL kuwa wakati huu wa uchaguzi, kampuni haitaegemea upande wowote hivyo uwajibikaji huo na weledi utasaidia vyombo vyote vya kampuni hiyo kuaminika kwa wadau wake.

“Hatutakiwi tuwe na tofauti na mamlaka. Tunachotaka ni kuwa huru kwa kila kitu tunachokifanya na siyo kuambiwa nini tufanye… tutakuwa wazi, watenda haki kwa kila mtu,” alisema Muganda huku akiwasihi wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya kampuni.

Katika hafla ya juzi iliyohudhuriwa na wanahisa, wasomaji, watangazaji, wafanyakazi wa MCL na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Muganda alisema atajikita katika kuhakikisha anafanikisha matarajio ya wanahisa wa kampuni hiyo.

Alisema ataweka mkazo katika kukuza vipaji vya vijana watakaosaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi na bara la Afrika kwa ujumla. “Mara nyingi sana tumekuwa hatutilii maanani uendelezaji wa mtaji wa nguvu kazi imara na yenye uweledi wa kutosha. Katika uongozi wangu nitafanya kila niwezalo kuendeleza vipaji na nguvu kazi kwa kuwashirikisha Watanzania kikamilifu,” alisema Muganda.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCL, Leonard Mususa aliipongeza kampuni hiyo kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuandika habari za Uchaguzi Mkuu kwa kina na haraka hasa wakati wa mchakato wa kumpata mgombea wa urais CCM.

Alisema wakati wa kutafuta tano bora hadi anavyolala hakuwa amepata habari yoyote ya matokeo, lakini alivyoamka asubuhi alikuta magazeti ya MCL yameandika kiundani habari hiyo.
Mususa hakusita kuendeleza na kilio cha kuiomba Serikali iliruhusu gazeti la The East African lianze tena kusambazwa nchini baada ya Serikali kulifungia Januari mwaka huu.

Mususa alisema soko la habari lina changomoto lukuki ambazo zinafahamika bayana na wadau wake. “Hadi sasa tunavyozungumza gazeti lililokuwa linapendwa nchini la The East African bado limefungiwa. Tunaamini kuwa Serikali italifungulia ili lianze kusambazwa tena nchini,” alisema.
“Nimeongea na wadau mbalimbali juu ya hilo na hata viongozi waliopo serikalini wanalipenda The East African…kwa chochote kilichotokea kisiwe tena sababu bali tunatakiwa kuyamaliza na kuwarudishia wasomaji gazeti walipendalo.”

Alisema kuna dalili za wazi kuwa hakuna kuaminiana kati ya vyombo habari na Serikali hivyo tasnia ya habari inatakiwa kujenga uaminifu na uhusiano mzuri na mamlaka kwa kuandika habari za kweli, haki na zisizoegemea upande wowote.

Mususa alisema MCL inataka kuongeza kiwango cha tabia ya kujisomea kwa kuwaomba wadau kutoa maoni juu ya masuala wanayopenda kuyasoma ili yaweze kuandikwa kwa ubora na uweledi wa hali ya juu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai alimuelezea Muganda kuwa ni “kiongozi mzuri ambaye tutanya naye kazi vizuri kama yule aliyetoka (Gitahi)”.




No comments: