Tishio la Dola la Kiislamu lainyemelea Kenya - LEKULE

Breaking

1 Jul 2016

Tishio la Dola la Kiislamu lainyemelea Kenya


Imebainika kwamba kwamba ushawishi wa kundi la Dola la Kiislamu Afrika Mashariki umeongezeka kwa kuwaandikisha vijana wa Kenya kuendesha mapambano ya jihadi nchi za nje na baadhi yao kurudi Kenya kuitishia nchi hiyo.
Mashirika ya ujasusi nchini Kenya yanakadiria kwamba takriban wanaume na wanawake 100 yumkini wakawa wamekwenda kujiunga na kundi la Dola la Kiislamu nchini Libya na Syria na kuzusha wasi wasi kwamba baadhi yao huenda wakarudi nchini humo kufanya mashambulizi kwa Kenya na katika vituo vya kigeni, katika nchi ambayo tayari ni muhanga wa mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika kila mara nchini humo.
Rashid Abdi mchambuzi mwandamizi katika Shirika la Kimataifa la Kushughulikia Mizozo ambalo ni jopo la ushauri lilioko katika mji mkuu wa Kenya Nairobi amesema "kwamba hivi sasa kuna tishio la kweli linaloikabili Kenya kutoka kundi la Dola la Kiislamu na hatari hiyo itazidi kuongezeka."
Tatizo la wafuasi wa itikadi kali ambao mara nyingi ni watu wenye shauku lakini wasiokuwa na mafunzo, kupatiwa mafunzo stadi ya kigaidi na kundi la Dola la Kiislamu na kurudi nyumbani kufanya mashambulizi ni tatizo ambalo tayari mataifa ya Ulaya yanakabiliana nalo na yumkini hivi karibuni likawa pia ni tatizo kwa Kenya.
Mshauri elekezi wa masuala ya usalama na afisa polisi wa zamani George Musamali ameliita hilo kuwa ni "bomu linasubiri kuripuka."Amesema watu kwenda Libya au Syria sio tatizo kwa Kenya tatizo ni kile watakachokifanya wakati watakaporudi.
Mashambulizi ya kigaidi sio tu kigeni Kenya
Shambulio la kwanza la kigaidi la Al- Qaeda nchini Kenya ilikuwa ni kuripuliwa kwa ubalozi wa Marekani hapo mwaka 1998 na hivi karibuni kabisa yalikuwa ni mauaji katika chuo kikuu cha Garissa mwaka jana lakini tishio la Dola la Kiislamu ni jipya na bado kueleweka vyema.
Hapo mwezi wa Machi wanaume wanne walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutaka kwenda Libya kuijunga na kundi la Dola la Kiislamu.
Baadae hapo mwezi wa Mei polisi ya Kenya ilitangaza kukamatwa kwa mwanafunzi wa udaktari,mke wake na shoga yake wanaotuhumiwa kuwaandikisha watu kujiunga na kundi la Dola la Kiislamu na kupanga shambulio la kibiolojia kwa kutumia anthrax.
Inasemekana wanafunzi wengine wawili wa udaktari wamekimbia.
Kukamatwa kwa silaha
Wiki tatu baadae polisi ya Kenya ilitangaza kukamatwa kwa wanachama wengine wawili wa mtandao wa kundi la Dola la Kiislamu ambao ulikuwa ukitaka kujipenyeza Kenya ili kuweza kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Wakenya wasiokuwa na hatia.
Polisi ilisema imegunduwa vitu ambayo hutumiwa na magaidi kutengeneza mabomu ya kienyeji pamoja na mikuki na mishale iliotiwa sumu.
Wakati baadhi ya wataalamu wanatupilia mbali ishara ya shambulio kubwa lainyemelea Kenya wanakiri kwamba kuna tishio la dhati la kundi la Dola la Kiislamu kupandikiza itikadi kali,kuandikisha watu kujiunga nalo na baadae kuwarudisha nyumbani.DW

No comments: