WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameitaka Polisi kutotumia
nguvu kubwa katika mambo yasiyokuwa na manufaa kwa wananchi ila nguvu
hizo zitumike kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa maslahi
mapana ya taifa.
Nchemba
ameyasema hayo juzi wakati akifunga mafunzo ya awali ya polisi na
uhamiaji, katika Shule ya Polisi Tanzania-Moshi, ambapo zaidi ya
wanafunzi 3,000 walihitimu mafunzo hayo.
Alisema
polisi ikifanya jitihada za kutokomeza biashara na matumizi ya dawa ya
kulevya, kila Mtanzania kwa kabila lake, kwa rangi yake na imani yake
atalipongeza jeshi hilo kwa kazi ambayo watakuwa wameifanya.
Alisema
wananchi hawataweza kulipongeza jeshi hilo kama litatumia nguvu kubwa
ya kupambana na masuala yasiyo na tija kwa wananchi, ambapo aliwataka
wahitimu wa mafunzo hayo kutekeleza kwa vitendo yale yote
waliyofundishwa kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo.
Nchemba
pia ameliagiza Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kinidhamu kwa
mujibu wa taratibu za jeshi hilo, askari Polisi wanaokiuka maadili ya
utendaji kazi wao, ikiwa ni pamoja na askari wanaobambikia watu kesi,
kupokea rushwa pamoja na kukamata raia kwa kutumia nguvu zisizostahili.
Alilaani
pia tabia ya wananchi kujichukuliwa sheria mkononi kama vile kuua watu
wasiokuwa na hatia kwa visingizio za imani za kishirikina, pamoja na
sheria kutofuatwa kwa watuhumiwa.
Mkuu
wa Shule ya Polisi Tanzania- Moshi, Matanga Mbushi, alisema wanafunzi
hao wamepewa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kufanya kazi kwa
ufanisi na kuongeza kuwa kati ya wanafuzi wanaohitimu, wanafunzi 99
wametimuliwa kutokana na makosa ya nidhamu na mimba.
No comments:
Post a Comment