Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali ambavyo haviendelezwi kutwaliwa ili kutolewa kwa wawekezaji wenye uwezo wa kuviendesha.
Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage ameyasema hayo jana
mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe.
Emmanuel Mwakasaka aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa juu ya
mwekezaji wa kiwanda cha nyuzi Tabora kwa kushindwa kuendeleza kiwanda
hicho.
“Wizara
kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na tathmini ya
viwanda vyote vilivyobinafsishwa na Serikali kikiwemo kiwanda cha nyuzi
cha Tabora ili kujiridhisha kama wawekezaji wa viwanda hivyo wanatimiza
matakwa ya mkataba na Serikali,” alifafanua Mhe. Mwijage.
Aliendelea
kwa kusema kuwa, ikiwa viwanda hivyo vitabainika kubadilishwa matumizi
yake au kutoendelezwa basi Serikali itavirudisha kwa watanzani ili
viweze kuendelezwa.
Aidha
Mhe. Mwijage amesema kuwa, kwa sasa mwitikio wa kuviendeleza viwanda
ambavyo vilikuwa havizalishi ni mzuri kwani viwanda vingi vimeanza
kufanya kazi lakini kwa wale ambao watashindwa kabisa kuviendeleza basi
viwanda hivyo vitarejeshwa kwa watanzania.
Vile vile
Mhe. Mwijage amesema kuwa dhana ya Serikali ya awamu ya Tano ya kujenga
uchumi wa viwanda inaenda pamoja na kurejesha Serikalini viwanda vyote
vilivyobinafsishwa lakini haviendelezwi ili vitolewe kwa wawekezaji
wengine.
Sambamba
na hayo Mhe. Mwijage amesema kuwa kufufua viwanda, hasa viwanda vya nguo
ni pamoja na wakulima wa pamba kulima zao hilo kwa wingi kwa ajili ya
uchakataji pamoja na kudhoofisha uingizaji wa nguo za mitumba nchini.
Wizara
hiyo inaendelea na kushawishi wawekezaji mbalimbali ili kujenga viwanda
vingi iwezekavyo kwa ajili ya uchakataji wa mazao yanayolimwa nchini
pamoja na mifugo.
No comments:
Post a Comment