Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta JOHN MAGUFULI amewahimiza viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania- BAKWATA- waendelee kuombea amani katika taifa na kukemea ipasavyo vitendo vya uhalifu katika jamii ya Kitanzania.
Kauli
hiyo ya Rais imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN kwa niaba ya Rais katika tafrija ya futari
iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania- BAKWATA- katika uwanja
wa shule ya sekondari ya KINONDONI MUSLIM jijini Dar es Salaam.
Rais
Magufuli amesema jamii yeyote inayolelewa na kukua katika misingi ya
kufuata maandiko ya Mwenyezi Mungu ni vigumu kujiingiza kirahisi katika
vitendo vinavyomchukiza Mungu vikiwemo vitendo vya uhalifu.
Rais MAGUFULI pia amewatakia kheri waumini wote wa dini ya kiislamu kote nchini katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa
upande wake, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh ABUBAKAR ZUBEIR ameipongeza
serikali kwa hatua inazochukua katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu
hapa nchini na kusisisita kuwa Viongozi wa BAKWATA na wataendelea
kushirikiana na serikali katika kukemea vitendo viovu katika jamii kama
hatua ya kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinakoma hapa nchini.
Mufti
wa Tanzania pia ametoa rai kwa waislamu wote nchini wadumishe
umoja,upendo na mshikamano miongoni mwao katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu
wa Ramadhani na hata baada ya mfungo kama kitabu kitukufu cha QUR’AN
kinavyoelekeza.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais.
No comments:
Post a Comment