Singida Washukuru kuwa wa Kwanza Mgawo wa Milioni 50/- za Magufuli - LEKULE

Breaking

10 Apr 2016

Singida Washukuru kuwa wa Kwanza Mgawo wa Milioni 50/- za Magufuli



Mbunge  wa Viti Maalumu, Aysharose Matembe (CCM), amesema vijana na wanawake mkoani Singida, wameishukuru Serikali kwa kuchagua mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa 10 ya kwanza itakayonufaika na mgawo wa Sh milioni 50 kila kijiji na kila mtaa.

Matembe amesema wako tayari kuzitumia kwa uangalifu fedha hizo kwa kuhakikisha wanaunda vikundi vyenye malengo madhubuti ya kujenga ili wajikwamue kiuchumi.

Mbunge huyo jana alisema Singida ni miongoni mwa mikoa yenye rasilimali nyingi, ikiwemo ardhi yenye rutuba ambayo kwa kiasi kikubwa wananchi wanaitumia kujishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali yanayochangia kukua kwa pato la Taifa.

Alisema amezungumza na wananchi hao ambapo walikiri fedha hizo kuwa na mchango chanya kwa maendeleo ya mkoa na kaya zao, hivyo kila mtendaji atakayehusika kwa namna moja au nyingine na fedha hizo, anapaswa kuwa mwadilifu ili ziwafikie walengwa kwa wakati.


“Kutolewa kwa hizi fedha ni kama kupatikana kwa maji jangwani kwa vijana na wanawake wa Singida, kwa nyakati tofauti nimezungumza nao na wananipa salamu kuishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuieleza kwamba wamejipanga kunufaika nazo.

No comments: