Profesa Muhongo Asema Kitendo Cha Marekani Kusitisha Misaada ya MCC Hakitaathiri Miradi ya REA ya usambazaji wa Umeme vijijini - LEKULE

Breaking

1 Apr 2016

Profesa Muhongo Asema Kitendo Cha Marekani Kusitisha Misaada ya MCC Hakitaathiri Miradi ya REA ya usambazaji wa Umeme vijijini


Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo amesema kuwa kwa   Tanzania  kutopatiwa  fedha na Marekani  kupitia Mfuko wa  Maendeleo  ya Changamoto za Milenia (MCC) ambazo ni Dola za Marekani  milioni 472 kwa ajili ya miradi ya  barabara,  maji na umeme hazitaathiri  miradi ya usambazaji umeme  vijijini inayofadhiliwa na  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA).

Aliyasema hayo  jijini Dar es salaam wakati  akifanya majumuisho  ya vikao vyake na wakandarasi wanaosambaza umeme  vijijini  ambavyo vilianza tarehe  29 Machi, 2016 na kuhudhuriwa na watendaji wa Wizara, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na REA.

Profesa Muhongo alisema kuwa fedha hizo zilikuwa haziendi moja kwa moja katika mfuko wa REA wala serikali kuu kama inavyodaiwa na watu wengi.

“Zile fedha za MCC tulikuwa tunakaa na MCC, tunasema bwana katusaidie kusambaza umeme mfano Shinyanga, kwa hiyo anachukua zile fedha zake anaenda na wakandarasi wake moja kwa moja Shinyanga, huku miradi ya REA ikiendela kama ilivyopangwa, ” alisema Profesa Muhongo.

Alisema kuwa miradi ya MCC ilikuwa ikisaidia juhudi za serikali katika kusambaza umeme   vijijini na mijini lakini fedha hizo zilikuwa hazipelekwi  REA.

Alisisitiza kuwa kabla ya MCC kuanza kutoa fedha za kuendeleza miradi ya umeme, serikali  tayari ilikwishaanza kusambaza  nishati hiyo kwa wananchi na kwamba   kuna wadau mbalimbali wanaochangia  miradi hiyo na hata kama wasipochangia, jukumu la serikali  la  kuwasambazia wananchi wake  umeme linabaki kuwa pale pale.

“Isichukuliwe kwamba fulani asipochangia, sasa taifa zima miradi yake imekufa, hivyo dhana ya kusema kwamba fedha hizo zilikuwa zinapelekwa REA ni upotoshwaji wa hali ya juu, kwamba REA itaathirika kwa kukosa hizo  fedha si kweli,” alisema Profesa Muhongo.

Akielezea utekelezaji wa miradi ya REA awamu ya pili, Profesa Muhongo alisema awali jumla ya shilingi bilioni 881 zilitengwa lakini zikaongezeka shilingi bilioni 60 ambapo  hadi kukamilika kwa awamu hiyo ya pili   jumla ya vijiji 2500 vinatarajiwa kupata umeme, huku wateja wa awali 250, 000   kuunganishwa na huduma hiyo hadi kufikia mwezi Juni, mwaka huu ambao ni ukomo wa utekelezaji wa awamu hiyo.

Kuhusu tathmini ya wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema kuwa wakandarasi wengi wametekeleza miradi hiyo kwa  asilimia kati ya 75 na  85, huku wengine wakivuka wastani wa REA  ambao ni asilimia 87.

Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alitoa miezi miwili kwa wakandarasi ambao hawajakamilisha  miradi na kusisitiza miradi yote kukamilishwa mwezi Mei au  Juni 15, mwaka huu  kabla ya kuanza kwa awamu ya tatu inayotarajiwa kuanza ifikapo Julai mosi mwaka huu.

Aliongeza kuwa katika  utekelezaji wa miradi ya umeme  vijijini, serikali imebaini kuwa  wapo wakandarasi wanaotumia  vifaa hafifu kama  transfoma na nguzo na kusisitiza  ukaguzi kufanyika na kampuni itakayobainika kutumia vifaa hafifu itafutwa mara moja kabla  ya awamu  ya tatu.

Ili kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi, Profesa Muhongo aliitaka  TANESCO kwa kushirikiana na Wizara  kuhamasisha wananchi hasa waishio  vijijini  kujiunga na huduma ya umeme,  na  TANESCO kusogeza  huduma  karibu na wananchi ili kuepusha wananchi  kusafiri umbali mrefu  kufuata huduma ya kuunganishiwa umeme au changamoto nyingine zinazotokana na nishati hiyo.

Akizungumzia kuhusu malipo ya wakandarasi hao, Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imeendelea kulipa wakandarasi wote kwa wakati kulingana kazi  zinazofanyika.


Wakati huo huo Profesa Muhongo alisema kuwa mitambo ya kuzalisha umeme  kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I  kwa sasa inazalisha Megawati 150 na kuongeza kuwa malipo kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya Kinyerezi II inayojengwa na kampuni ya Sumitomo kutoka nchini Japan yameshakamilika

No comments: