Waziri Mkuu kuwa mgeni rasmi harambee ya shule ya Sekondari ya Iyunga - LEKULE

Breaking

18 Mar 2016

Waziri Mkuu kuwa mgeni rasmi harambee ya shule ya Sekondari ya Iyunga

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee itakafanyika kesho katika ukumbi wa Ubungo Plaza kwa ajili ya kuchangia fedha zitakazowezesha kukarabati mabweni manne ya shule ya Sekondari ya Ufundi ya Iyunga yaliyoungua hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Nyerembe Munasa Sabi amesema kuwa wameamua kuomba nguvu kutoka kwa wadau wa elimu na watanzania kwa ujumla kujumuika katika kuchangia shule ya sekondari ya ufundi Iyunga ili waweze kukarabati mabweni yaliyoungua kwa moto.

“ Hadi sasa takribani wanafunzi 421 hawana mahala pa kulala kutokana na kuteketea kwa mabweni na kwa kushirikiana na TAMISEMI tumeamua kusitiza masomo kuanzia tarehe11 March hadi tarehe 01 Aprili ili kupisha ukarabati wa mabweni”

“ Tumeanza ujenzi wa baadhi ya miundombinu iliyoteketea na mabweni ikiwa ni jitihada za wadau mbalimbali waliochangia kutoka Mbeya na nawasihi wanambeya wale waliosoma shule ya Iyunga na shule za Mbeya na watanzania kwa ujumla kujitokeza kesho katika harambee hii” Alisema

Mhe. Nyerembe Munasa Sabi aneongeza kuwa wamepokea michango mbalimbli kutoka kwa wadau wakiwemo Mbeya Cement waliotoa mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya ujenzi na kwa sasa mahitaji yaliyopo ni takribani Shillingi million 770 ili kukarabati na kujenga majengo mapya kwa ajili ya shule hiyo.

Shule ya Sekondari ya  Ufundi Iyunga yenye wanafunzi takribani 9970 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita imekumbwa na majanga ya moto ambayo yamesababisha athari kwa  watoto kutoendelea na masomo na uharibifu wa miundombinu ila Serikali kupitia TAMISEMI na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya wamejipanga kukusanya  fedha kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa shule hiyo.

No comments: