Waziri Kitwanga Asema Wabunge Wataendelea Kukamatwa Kama Hawatafuata Sheria za Nchi. - LEKULE

Breaking

18 Mar 2016

Waziri Kitwanga Asema Wabunge Wataendelea Kukamatwa Kama Hawatafuata Sheria za Nchi.


Wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akidai wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wanakamatwa bila sababu za msingi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema hakuna mtu anayekamatwa bila sababu na kwamba yeyote atakayebainika kufanya kosa, atasweka ndani bila kujali chama chake.

Machi Mosi, mwaka huu, Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wabunge na madiwani kutoka Ukawa, wanadhalilishwa na kunyanyaswa kila kona nchini na kwamba hizo ni juhudi za kurudisha nyuma maendeleo ya kazi za viongozi hao.

Hivi karibuni, Waziri Kitwanga alisema kuwa wananchi watambue kwamba askari polisi ni rafiki wa raia mwema, hivyo hawawezi kumkamata mtu asiyetenda kosa.

“Nitamshangaa askari polisi, mtu anatenda kosa pale wasimkamate eti kwa sababu tu ni mbunge wa upinzani. Awe wa CCM, awe wa upinzani watakamatwa, mimi nimeshawaeleza.

“Nimeshawaeleza wazi kabisa, mimi nitasimamia haki tu, tofauti na hapo hapana, wewe ungeona yule mama alivyopigwa na wabunge(Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando) inaumiza sana. Nilichukia sana lakini hata sikuwasemesha polisi, nilikaa kimiya tu niwaone watafanyaje.


“Niliamua kuwapima, ‘infact’ (kwa kweli) hawa watu hata dhamana wasingewapa kwa kitendo hicho,” alisema Kitwanga

No comments: