Waliokula mishahara HEWA Singida kusherehekea siku ya Wajinga Rumande - LEKULE

Breaking

26 Mar 2016

Waliokula mishahara HEWA Singida kusherehekea siku ya Wajinga Rumande


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza mamlaka zinazohusika kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu watakaobainika kutafuna fedha za mishahara hewa kabla ya mwezi huu kumalizika.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha kufahamiana kilichohudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa idara ya sekretarieti ya mkoa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ofisini kwake.

Katika hotuba yake fupi na ambayo haikuwa na mbwembwe za kisiasa, alisema uhakiki uliofanyika hivi karibuni mkoani humo ulibainika kuwa na wafanyakazi hewa wengi, jambo linaloonyesha kuwapo kwa ubadhirifu wa kiwango cha juu cha fedha za umma.

“Naagiza kila mmoja wenu akaangalie kwenye taasisi yake iwapo wafanyakazi wanaolipwa mishahara ndiyo hao waliopo kazini au la. Kuna madai wastaafu, waliohama na hata watumishi waliokufa mishahara yao bado inalipwa hadi hivi leo,”alisema.

“Iwapo itagundulika kuwa kuna watu walioshiriki katika ulaji huo wa fedha za umma, wakamatwe mara moja ifikapo Aprili Mosi, mwaka huu na kufikishwa kunakohusika haraka iwezekanavyo ili sheria ichukue mkondo wake.”

Mtigumwe aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa watumishi walio chini yao kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

“Haiwezekani mtu atoke kijijini kisha arudi bila kuhudumiwa, lazima kuwahi kazini na kukaa hadi mwisho wa saa za kazi,” alisema.


Pia, alisisitiza umuhimu wa kila taasisi ya Serikali mkoani humo kufungua kitabu cha kero za wananchi na kuhakikisha zinaorodheshwa na kuonyesha hatua halisi iliyofikiwa katika kuzishughulikia. 

No comments: