SHIRIKA LA UMEME ZANZIBAR (ZEKO) LAKANUSHA SHUTMA ZA KUSITISHA KUUZA UMEME VISIWANI HUMO - LEKULE

Breaking

5 Mar 2016

SHIRIKA LA UMEME ZANZIBAR (ZEKO) LAKANUSHA SHUTMA ZA KUSITISHA KUUZA UMEME VISIWANI HUMO

ZEKO
Meneja Mkuu Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) Hassan Ali Mbarouk alipokuwa akizungumza na wandishi wa Habari  (Hawapo pichani) kuhusu uvumi ulionea kwamba litasitisha  huduma ya kuuza umeme kwa siku kadhaa katika Mkutano uliofanyika Ofisi za ZECO ziliopo Bulioni Mjini Zanzibar mapema jana Machi 4.2016.
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limekanusha uvumi ulionea kwamba litasitisha huduma ya kuuza umeme kwa siku kadhaa na kusababisha hofu kwa wateja na kupelekea msongamano katika vituo vya kununulia umeme vya Shirika hilo katika siku za karibuni.
Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake Makadara, Meneja Mkuu wa ZECO ndugu Hassan Ali Mbarouk amesema kuongezeka kwa wateja katika vituo vya kuuzia umeme vya Shirika hilo kumesababishwa kukosekana huduma hiyo kwa kutumia simu za mkononi za Zantel kwa Easy pesa.
Ndugu Mbarouk amesema huduma ya kununua umeme katika vituo vyote vya ZECO itaendelea kama kawaida kwa siku zote na hakutakuwa na kuzimika wala kusita kuuza umeme katika vituo hivyo.
Hata hivyo amesema huduma ya kununua umeme kwa kutumia simu za mkononi kwa njia ya easy pesa itaendelea kukosekana na amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati huu ambapo ZECO na Zantel wanaendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo lililojitokeza.
Amesema kukosekana huduma hiyo kwa njia ya easy pesa imesababishwa na mfumo huo kupata matatizo kuanzia tarehe 20 mwezi uliopita.
Amewahakikisha watumiaji wa umeme kwamba tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi katika kipindi kifupi kijacho kwani mkataba wa mwanzo wa miaka miwili wa ZECO na Zantel utakapo malizika mkataba mpya utatoa fursa kwa mashirika mengine ya simu kuingia mkataba wa kuuza umeme.
Akizungumzia zoezi linaloendelea la kubadilisha mita za zamani na kuweka mita za Tukuza, Menaja Mkuu amesema Shirika limepanga itakapofika mwishoni mwa mwaka 2017 wateja wote wa umeme watakuwa wanatumia mita za Tukuza.
Amesema pamoja na mafanikio makubwa waliyopata ya kubadilisha mita za zamani wanawasi wasi kwa baadhi ya wateja wasiowaaminifu kuzihujumu mita za Tukuza na kulikosesha fedha shirika kwani mita hizo zinachukua muda mkubwa kukaguliwa baada ya kuwekwa tafauti na mita za zamani ambazo hukaguliwa kila mwezi.
Meneja Biashara wa Shirika la umeme Zanzibar ndugu Thabit Salum Khamis amewaeleza waandishi wa habari kuwa usambazaji umeme katika visiwa vya Unguja na Pemba umefikia asilimia 86 lakini watumiaji umeme ni chini ya asilima 50.
Ndugu Thabit amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kutumia zaidi umeme kwani ni rahisi kwa matumizi ya nyumbani ikilinganishwa na nishati ya kuni na mkaa.

No comments: