Sakata la Umeya Dar: Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea Apandishwa Kizimbani. - LEKULE

Breaking

11 Mar 2016

Sakata la Umeya Dar: Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea Apandishwa Kizimbani.


MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea na Manase Mjema, Diwani wa Kimanga wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo asubuhi  na kusomewa shitaka la kudhuru mwili  ambapo wote wawili wamekana shitaka hilo.

Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kumshambulia Terresia Mmbaando, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam  tarehe 27 Februari 2016.

Kubenea anatajwa kuwa ni mtuhumiwa namba sita ambapo Manase akiwa mtuhumiwa namba nne.

Mmbando alikuwa mwenyekiti wa mkutano wa kumchagua Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliofanyika kwenye Ukumbu wa Kareem Jee na baadaye kuahirishwa hatua ambayo iliibua malumbano.

Mbele ya Cyprian Mheka, Hakimi Mkazi Kisutu washitakiwa hao walikana kosa hilo ambapo hakimu alighairisha kesi hiyo mpaka tarehe 16 Machi mwaka huu.

Hata hivyo, Hakimu Mkeha aliwataka watuhumiwa hao kujidhamini wenyewe kwa dhamana ya Sh. 2,000,000 sharti ambalo wamelitekeleza.

Jana asubuhi kwenye mahakama hiyo Kubenea akihudhuria kesi yake dhidi ya Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, alikamatwa na Jeshi la Polisi na kuwekwa chini ya ulinzi.


Kubenea na Manase wameunganishwa kwenye kesi hiyo ambapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamni awali  ni Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Mwita Waitara, Mbunge wa Ukonga na madiwani wawili jumla yao ikiwa ni watuhumiwa sita.

No comments: