Rais Magufuli Ampongeza Francis Cheka kwa Kutwaa ubingwa wa Mabara wa Uzito wa Super-Middle - LEKULE

Breaking

5 Mar 2016

Rais Magufuli Ampongeza Francis Cheka kwa Kutwaa ubingwa wa Mabara wa Uzito wa Super-Middle



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amempongeza bondia Francis “SMG” Cheka kwa kutwaa ubingwa wa Mabara wa uzito wa Super-Middle wa chama cha WBF baada ya kumtwanga kwa pointi bondia Mserbia, Geard Ajetovic.

Cheka alimchapa Ajetovic kwa ushindi wa majaji wote wa tatu katika pambano gumu lililofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club.

Akitoa pongezi hizo jana, Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema kuwa Rais amefuraishwa sana na ushindi wa Cheka ambao umeipa heshima nchi katika medani ya michezo ndani na nje ya mipaka yake.

Waziri Nnauye alisema kuwa serikali imeweka utaratibu wa kuwapongeza wanamichezo wanaofanya vyema kimataifa ili kuleta hamasa kwa wengine na wale wanoafanya vizuri kuongeza bidii.

“Cheka umefanya mambo makubwa sana, umeiletea sifa Tanzania na Rais amefuraishwa sana, naomba kuongeza bidii na wengine kufuata nyayo zako, nimefurahi kusikia kuwa mdogo wako, Cosmas naye ameshinda ubingwa wa Afrika, nampongeza sana,” alisema Nnauye.

Katika hafla hiyo, Serikali ilimpa cheti cha pongezi Francis Cheka na kumtaka kuzidi kuitangaza nchi kupitia mchezo huo ambao ni wa kwanza katika historia ya Tanzania kuleta heshima. “Serikali inaahidi kusaidia mchezo na mabondia ili kufikia maendeleo ya juu kabisa,”alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Cheka aliipongeza serikali na kutambua mchango wake katika kuleta sifa ya nchi hii na kuahidi kuleta mikanda mingi ya ubingwa wa dunia.

“Nimefurahi kutambuliwa na serikali, nimepata hamasa kubwa sana, naahidi kufanya mambo makubwa katika mchezo huu,” alisema.
 
Mkurugenzi wa Advanced Security, Juma Ndambile ambaye ni meneja wa Cheka alisema kuwa wamefarijika sana kupata pongezi za serikali na kuahidi kuandaa mapambano mengi ya Cheka kwa mabondia wan je ya chi katika mapambano ya ubingwa wa Dunia.

No comments: