Mkuu wa Wilaya Aagiza kushushwa Vyeo Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari Zilizofanya Vibaya Katika Matokea ya Mtihani - LEKULE

Breaking

31 Mar 2016

Mkuu wa Wilaya Aagiza kushushwa Vyeo Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari Zilizofanya Vibaya Katika Matokea ya Mtihani


Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho ameagiza kushushwa vyeo wakuu wa shule zote za msingi na sekondari katika wilaya hiyo, ambao shule zao zimefanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na sekondari mwaka 2015/2016.

Aidha amewataka wenyeviti na wajumbe wa bodi za shule kujipima uhalali wao kama wana sifa ya kuendelea kuwemo katika nyadhifa zao, kutokana na matokeo mabaya yaliyopata shule wanazozisimamia ambayo yameitia aibu wilaya hiyo.

Alisema wenyeviti na wajumbe wa bodi ni lazima waachie ngazi kwani shule zao zimefanya vibaya na imeonekana sababu mojawapo ya kufanya vibaya kwa shule hizo ni walimu kutowajibika.

Alisema wameshindwa kuwafuatilia na kushindwa kushirikiana na wazazi kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili shule zao.

Nalicho alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakuu wa shule nne za sekondari, wajumbe na wenyeviti wa bodi za shule hizo zilizofanya vibaya katika matokeo ya kumaliza elimu ya sekondari mwaka uliopita.

Alikutana nao katika kikao maalumu cha kazi na baadhi ya watumishi wa kata ya Lusewa kilicholenga kutafuta majawabu juu ya kero zinazowakabili wakazi wa kata hiyo.

 Shule zilizofanya vibaya katika matokeo hayo ni Lusewa, Msisima, Kwizombe na Matepwende.

Aliwataka walimu na wakuu wa shule hizo kuongeza juhudi katika kuwasaidia watoto madarasani ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

“Sitakubali mwaka ujao kuona shule zenu zinaendelea kushika mkia, ninyi ndiyo chanzo cha wilaya yetu kushika nafasi ya pili kutoka mwisho katika matokeo ya mitihani ya mwaka jana. Nataka muongeze juhudi katika kazi zenu, tumieni muda mwingi kuwafundisha hawa watoto madarasani, badala ya kutumia muda wenu kwa ajili ya kufanya anasa,” alisema Nalicho.

Alisema suala la elimu ni muhimu katika maisha ya binadamu kwani hakuna anayeweza kufanikiwa katika maisha yake kama hajakwenda shule.



Aliwasisitiza kuwa muda umefika kwa wakazi wa kata hiyo kuona aibu na matokeo hayo, badala yake wahimize watoto wao kupenda shule kwa kuwa elimu ndiyo urithi bora kwa mtoto.

No comments: