Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka
MKURUGENZI
wa Halmashauri ya wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, John Aloyce
amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo kushindwa
kuisimamia halmashuari hiyo na kusababisha kuwepo kwa migogoro ya mara
kwa mara kati ya madiwani na watendaji.
Uamuzi
huo umechukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka katika kikao
cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana mjini
Langangabilili wilayani humo.
Mbali
na uamuzi huo, amefuta posho zote kwa wakuu wa idara na vitengo katika
halmashauri zote zilizoko mkoani hapa wanaoingia katika vikao vya
madiwani.
Vikao
hivyo ni pamoja na Baraza na kamati za halmashauri kwa madai kuwa
hazina tija yoyote, na kuelekeza fedha hizo zilizotengwa zifanye kazi
nyingine za maendeleo kama vile utengenezaji wa madawati.
Alisema
alipata malalamiko dhidi ya Mkurugenzi huyo kupitia wajumbe wa Kamati
ya Fedha na Mipango wa halmashauri hiyo waliofika ofisini kwake, hivyo
kuamua kuitisha kikao hicho cha dharura ili kuyasikiliza.
Katika
kikao hicho madiwani hao walisema serikali ilitoa Sh milioni 450 kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika halmashauri hiyo lakini
kazi hiyo haikufanyika, wanapohoji na kutoa uamuzi umekuwa haufanyi
kazi.
“Wilaya
yetu ni mpya na katika kuondoa tatizo la watumishi wa halmashauri hii
kuishi mbali na makao makuu ya wilaya tuliamua kuanza ujenzi wa nyumba
za watumishi na tukaletewa Sh milioni 450. Lakini kila tunapohoji
matumizi ya fedha hizo hatupatiwi majibu na tunapomwagiza Mkurugenzi
atuletee hakubaliani na maamuzi yetu,”alisema Kuzenza William (CCM),
ambaye ni Diwani wa Kata ya Zagayu.
Walisema
kuwa hata mapato ya ndani yanayopatikana hayafahamiki licha ya kuwepo
kwa ushuru wa mazao mchanganyiko haulipwi na wafanyabiashara walio
wengi, hivyo kusababisha shughuli nyingi za halmashauri kukwama na kuzua
migogoro ya mara kati ya madiwani na ofisi ya Mkurugenzi.
“Mapato
ya ndani hayafahamiki kabisa kuwa ni kiasi gani cha fedha kimepatikana,
maana hatusomewi na inaonekana hata ushuru wa mazao mchanganyiko
wafanyabiashara hawalipi hii timu ya mkurugenzi inayosimamia mapato sina
imani nayo,” alisema Diwani Kata ya Lugulu, Robert Jongela.
Mwenyekiti
wa halmashauri hiyo, Daud Nyalamu alisema madiwani wa halmashauri hiyo
wanaonekana hawana uamuzi kwani waliagiza kuwa vifaa vyenye thamani ya
Sh milioni 320 vilivyokopwa na halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa
maabara 35 za shule za sekondari vifanye kazi, lakini hadi sasa hakuna
kilichofanyika na vingi vimeharibika.
“Tulikopa
benki Sh milioni 320 kwa ajili ya ujenzi wa maabara 35 zilizoko katika
halmashauri yetu, vifaa vimenunuliwa lakini hadi sasa vimesambazwa
maeneo mbalimbali havijafanyiwa kazi. Vimeharibika kwani saruji imeganda
na mbao zimepinda na hazifai kwa ujenzi. Hii inatokana na uzembe wa
Mkurugenzi wetu na kila kukicha halmashauri inadaiwa hadi madiwani
hatulipwi stahili zetu,” alisema.
Akizungumzia
tuhuma dhidi yake, Aloyce alisema tangu ateuliwe kuwa Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo miezi sita iliyopita alikuta Sh milioni 126 zilizokuwa
zimebaki katika ujenzi wa nyumba za watumishi.
“Mimi
wakati nafika katika halmashauri hii nilikuta kati ya Sh milioni 450 za
ujenzi wa nyumba za watumishi zilikuwa zimebaki Sh milioni 126, tulikaa
na wakuu wa idara tukaamua tuzikope na kujenga ukumbi ukizingatia ya
kuwa tulikuwa tunaelekea uchaguzi mkuu hivyo tungeshindwa mahali pa
kukusanyia matokeo ya kura,” alisema.
Alisema
licha ya tuhuma mbalimbali dhidi ya halmashauri hiyo, iliundwa tume
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuzichunguza lakini hadi sasa
hawajawaletea majibu, hivyo kuomba iundwe tume huru kutoka nje ya mkoa
ili kuweza kuzichunguza tuhuma zilizotajwa na madiwani dhidi yake na
ikibainika yuko tayari kuachia ngazi
No comments:
Post a Comment