Jamii Forums Wakimbilia Mahakamani....Wadai Kushinikizwa na Jeshi la Polisi Kutoa Siri za Wachangiaji wao - LEKULE

Breaking

5 Mar 2016

Jamii Forums Wakimbilia Mahakamani....Wadai Kushinikizwa na Jeshi la Polisi Kutoa Siri za Wachangiaji wao



Kampuni ya Jamii Media ambayo ni wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya Jamii Forums na FikraPevu, wamefungua kesi ya Katiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga amri waliyopewa na polisi ya kutoa taarifa binafsi za wanachama wao.

Akizungumza baada ya kufungua kesi hiyo jana, Wakili wa Jamii Media, Shukuru Mkwafu alisema lengo lao ni kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya kwani vinasababisha kuvunjwa kwa haki za msingi za Watanzania watumiao mitandao.

Wakili Mkwafu alisema ili kulinda masilahi ya umma, lazima vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vizingatiwe.

Alisema Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015, inakiuka haki ya kikatiba namba 16 inayoruhusu kuwapo na hali ya faragha na kifungu namba 18 kinazungumzia uhuru wa kujieleza.

Mmiliki wa tovuti hizo, Maxence Melo alisema kwa takriban miezi mitatu iliyopita Polisi imekuwa ikiwashinikiza kwa njia ya barua kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake wanaoonekana kutoa taarifa zile ambazo kwa namna moja au nyingine, zinaibua ufisadi mkubwa na ukwepaji kodi.

Melo alisema katika kuhakikisha inasimamia usiri wa wateja wake, wamekuwa wakihoji sheria inayofuatwa kwenye mashinikizo hayo na kutaka kujua vifungu vya sheria ambavyo wadau wa mtandao huo wamevivunja, bila kupewa maelezo yanayoridhisha zaidi ya kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama hawatatoa ushirikiano kwa Polisi.

Mmoja wa Mawakili wanaosimamia kesi hiyo itakayotajwa tena Machi 9, Benedict Alex alisema ni vyema polisi wakaweka wazi mlalamikaji katika madai yao badala ya kutoa vitisho bila kutoa ufafanuzi. 

No comments: