Watu 21 Watiwa Mbaroni kwa Mauaji ya Kondoo Na Mbuzi Mvomero - LEKULE

Breaking

11 Feb 2016

Watu 21 Watiwa Mbaroni kwa Mauaji ya Kondoo Na Mbuzi Mvomero


WENYEVITI wa Serikali za vijiji vya Mkindo, Patrick Longomeza (52) na mwenzake wa Dihombo, Christian Thomas (50) pamoja na wananchi wengine 19 wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujeruhi mifugo mali ya mwanamke mfugaji wa Kimasai, Katepoi Nuru (36) wa Kijiji cha Kambala wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro.

Mbali na wenyeviti wa vijiji hivyo, pia Polisi wamemtia mbaroni kinara wa uhamasishaji vijana wa kimasai kuwapiga na kuwajeruhi wakulima wanaolima katika Bonde la Mgongola, Kashu Moreto (68) kwa tuhuma za kulisha mazao na kumjeruhi mguu wa kulia, mkulima Ramadhan Juma (19), mkazi wa Dihombo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la awali lililotokea Februari 7, mwaka huu mchana katika Kijiji cha Kambala.

Alisema kabla ya kukatwa kwa mifugo ya mwanamke huyo, kundi la ng’ombe zaidi ya 50 likiwa na wachungaji zaidi ya watatu wa Kimasai walilisha shamba la mpunga ekari moja la mkulima Rajab Issa (31) aliyewazuia na ghafla walijitokeza vijana wanaosadikiwa kuwa ni Morani wa kimasai na kuwachukua ng’ombe hao kwa nguvu.

Aliwataja wengine waliotiwa mbaroni mbali na wenyeviti hao ni Issa Ally (66), Hussein Said (25), Juhudi Amimu (25), Emily Pascal (40) na Mkude Milikioni (25) ambao wote ni wakazi wa Kijiji cha Mkindo.

Wengine waliokamatwa ni Ally Bakari (25), Gerald Mbegu (22), Miraji Noras (22), Mengi Mbegu (32), Kudura Abdi (35), na wanawake wawili Angelina Sadiki (20), Hadija Msanga (30), wote wakazi wa Kijiji cha Mkindo.

Pia wamo Mustafa Malugo (35), Charles Moris (40), Amset Alfred (42), Hassan Mohamed (46) pamoja na Hapifan Paulo ambao wote hao ni kutoka katika Kijiji cha Dihombo wilayani Mvomero.

Kamanda Paulo alisema baada ya vijana hao wa kimasai kuingia kulisha katika shamba la Issa, alijaribu kuwazuia, lakini ghalfa walijitokeza vijana wanaosadikiwa kuwa ni morani wa kimasai na kuwachukua ng’ombe hao kwa nguvu, na mkulima huyo alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mvomero.

Lakini alisema Februari 8, mwaka huu mchana wakati tukio hilo likishughulikiwa, kikundi cha watu kilivamia nyumbani kwa Nuru Kipande (76) na kumkuta kumkuta Ketepoi Nuru (36) akiwa nyumbani huku mifugo aina ya mbuzi, kondoo na ndama wakiwa malishoni.

Kwa mujibu wa Kamanda, kundi hilo lilinyang’anya mifugo hiyo na kisha kumnyang’anya mwanamke huyo simu yake ya mkononi ili asiombe msaada na kisha kuipeleka mifugo hiyo porini na kuanza kuikatakata kwa vitu vyenye ncha kali .


Kamanda alisema watuhumiwa waliokamatwa wanaendelea kuhojiwa na wengine kutafutwa na wote waliohusika katika tukio hilo watafikishwa mahakamani, na kutoa onyo kwa watu wote kuacha kujichukulia sheria mkononi.

No comments: