Watu 20 Wafikishwa Mahakamani Kwa Kukatakata Mapanga Mbuzi Na Kondoo Mvomero - LEKULE

Breaking

13 Feb 2016

Watu 20 Wafikishwa Mahakamani Kwa Kukatakata Mapanga Mbuzi Na Kondoo Mvomero



Wakulima 20 wamefikishwa mahakamani kujibu shitaka la kukatakata na kuua mifugo, huku mfugaji mmoja akitakiwa kujibu mashtaka matatu ya kuharibu mali, kulisha mifugo kwenye shamba la mpunga na kumshambulia mmiliki wa shamba.

Washitakiwa hao walifikishwa kwenye mahakama mbili tofauti; wakulima walipanda kizimba cha Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, huku wafugaji wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Ivan Msaki wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.

Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Regina Futakamba, wakili wa Serikali, Edger Bantulaki alidai kuwa Februari 8, wakulima hao kwa pamoja walikatakata mbuzi na kondoo wenye thamani ya Sh6,140,000 mali ya Ketepoi Nuru, mkazi wa kijiji cha Kambala wilayani Mvomero.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka hayo na hivyo kurudishwa mahabusu kutokana na kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana. Kesi yao itatajwa tena Februari 25.

Ili wapewe dhamna washtakiwa hao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoishi mkoani Morogoro na kila mdhamini awe na kitambulisho pamoja na mali yenye thamani ya Sh3,070,000.

Mbele ya Hakimu Msaki, wakili huyo pia alimsomea mashtaka matatu Kasho Mereto, akidai kuwa alilisha mifugo kwenye shamba la mpunga na kuharibu mazao yenye thamani ya Sh300,000, kuharibu baiskeli na kumshambulia mmiliki wa shamba hilo, Rajabu Issa, mkazi wa kijiji cha Dihombo wilayani Mvomero.

Mfugaji huyo alikana shtaka na yuko nje kwa dhamana. Kesi hiyo itatajwa Februari 29. 

No comments: