Watu watatu wamekamatwa na polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuvamia Kituo cha Polisi cha Duthumi na kuvunja mlango kwa lengo la kuwatoa wenzao watatu wanaotuhumiwa kwa wizi wa mifugo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Graifton Mushi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 12.40 jioni.
Alisema polisi walilazimika kutumia silaha za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao.
Mushi alitaja silaha hizo kuwa ni mapanga, shoka na marungu. Hata hivyo, alisema wakati watu hao wanavamia kituo hicho watuhumiwa hao walishaondolewa kituoni hapo na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati. Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine; watu zaidi ya 20 wa Kitongoji cha Mazizini Kijiji cha Maseye Wilaya ya Morogoro wamevamia eneo la mwekezaji Ayubu Mngimbwa na kuteketeza vibanda vilivyokuwa na vifaa mbalimbali vya uchimbaji wa madini na kumshambulia kwa vipigo.
Kaimu Kamanda huyo alisema thamani ya vibanda na vifaa vilivyoteketezwa bado haijafahamika.
Alisema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro kati ya wananchi wa kitongoji hicho na mwekezaji anayedaiwa kutiririsha maji yenye kemikali za sumu.
No comments:
Post a Comment