Wabunge Wa CCM Wamgomea Magufuli - LEKULE

Breaking

4 Feb 2016

Wabunge Wa CCM Wamgomea Magufuli



Kikao cha siri cha wabunge wa CCM kilichoitishwa juzi usiku kujadili mipango ya Serikali kudhibiti matumizi, kimefanikiwa kukwamisha uamuzi wa kuzitaka halmashauri na mashirika ya umma kuingiza mapato yake yote kwenye mfuko mkuu.

Mpango huo, ambao pia ulipingwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani, ulilenga kuondoa utaratibu uliopo wa halmashauri, mashirika na taasisi za Serikali kukusanya mapato yake na kuzitumia na badala yake zilitakiwa ziingize mapato hayo kwenye mfuko mkuu na baadaye Serikali itoe fedha kulingana na bajeti inazopelekewa.

Juzi, katika mjadala wa mwongozo wa Mpango wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2016/17, wabunge hao walipinga uamuzi huo wakisema utaziua halmashauri na wakataka mashirika ambayo yanamilikiwa na Serikali ndiyo yapeleke fedha kwenye mfuko huo. 

Kutokana na mvutano huo, juzi usiku wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma, kujadili jambo hilo na kushauri libadilishwe ili kuziokoa halmashauri nchini.

Jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema  kuwa tayari Serikali imetoa maelezo.

“Tumetoa maelezo kuwa hatukumaanisha halmashauri wala mifuko ya hifadhi za jamii. Suala hili litayahusu mashirika ya umma pekee,”alisema Simbachawene.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wabunge hao walimbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwamba uamuzi huo utazifanya halmashauri kukosa fedha za kufanya miradi yake mbalimbali ikwame.

“Mkutano ulianza saa mbili usiku na kumalizika saa tano usiku. Tulichokubaliana na kufanyika kwa marekebisho ili halmashauri ziendelee na utaratibu kama wa awali, pia kuitaka Serikali kutoihusisha mifuko ya hifadhi za jamii katika suala hili,” alisema mbunge ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

“Fedha zitakazokwenda katika mfuko huo ni za mashirika kama Tanesco na Tanapa.Lengo hapo ni kuweka utaratibu mzuri wa matumizi kwamba shirika linaingiza fedha zake katika mfuko, likihitaji fedha litapelekewa kulingana na utaratibu utakaowekwa.”

Chanzo hicho  kilieleza kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii haitaguswa kwa sababu fedha zake ni za wanachama na hutumika kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali.

“Wabunge pia walihoji kama fedha hizo zitaweza kutoka katika mfuko huo na kuzifikia halmashauri katika kipindi hiki ambacho fedha nyingi zinashindwa kufika kwa wakati kutekeleza miradi ya maendeleo,”alisema mbunge mwingine.

Jana, katika mjadala wa mpango huo hakuna mbunge wa CCM wala wa Ukawa aliyegusia suala hilo, kitendo kinachotafsiriwa kuwa jambo hilo limeondolewa kabisa. 

Wachangia mjadala 
Akichangia mjadala wa mpango huo, Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi aliishauri Serikali kuachana na vyanzo vya mapato vilivyozoeleka, badala yake itafute vyanzo vipya.

Katika mpango huo, Serikali ilitaja baadhi ya vyanzo vyake vya ndani vya mapato kuwa ni kodi katika vinywaji mbalimbali, sigara, muda wa matumizi wa simu za mkononi na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). 

Katika eneo hilo imeweka uwekezako wa kukusanya Sh4 trilioni.“Watendaji wa Serikali lazima wajifunze kutoka katika taasisi ambazo zina vyanzo vingi vya mapato. Mapato yako mengi tu hata katika nyumba za kupanga na kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato zaidi,” alisema.

Mbunge wa Hanang’(CCM), Dk Mary Nagu alisema uchumi wa viwanda unategemea kilimo, mifugo na uvuvi na kuitaka Serikali kuhakikisha inatilia mkazo sekta hizo kwa maelezo kuwa itasaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Teonist alionyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mipango huo wa Serikali, kutokana na mawaziri wengi kufanya kazi kwa kutafuta sifa katika vyombo vya habari.

Alimtaja Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwamba anahusika katika uporaji wa viwanja vya wananchi. 

“Katika sekta ya ardhi kuna matatizo makubwa. Migogoro ya ardhi inarudisha nyuma maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa. Pale Dar es Salaam sasa mnavunja nyumba za watu wa mabondeni. Kutokana na zoezi hilo, zaidi ya watu 99, 000 watakuwa hawana makazi,” alisema.

Alisema kasi ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo ni ndogo na kwamba kwa kipindi cha miaka 15, Serikali imepunguza umasikini kwa asilimia 14 tu.

No comments: