Timuatimua yaanza Chadema Mkoani Mbeya - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 22 February 2016

Timuatimua yaanza Chadema Mkoani Mbeya


Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji ya wilaya hiyo wamevuliwa uongozi kwa kile kilichodaiwa kuwapo kwa msuguano miongoni mwao.
 
Uamuzi huo ulifikiwa usiku wa kuamkia jana kwenye kikao cha mashauriano kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Issa Said Mohamed.
 
Mohamed alipoulizwa kuhusu uamuzi huo, aligoma kulizungumzia kwa undani akidai hayo mambo ya ndani ya chama.
 
Hata hivyo, alikiri kusimamia kikao hicho ambacho kilianza saa 2.00 usiku na kumalizika saa 11.00 alfajiri.
 
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo Maghorofani jijini Mbeya.
 
Taarifa za ndani ya chama zilizopatikana jana asubuhi, zilidai kuwa awali, wajumbe walimuomba makamu mwenyekiti huyo kufika jijini hapa na kuitisha kikao hicho kujadili msuguano uliopo.
 
Mmoja wa wajumbe waliokuwapo kwenye kikao hicho ambaye hakutaka kuandikwa  jina , alisema kuliibuka malumbano makali huku wajumbe wakinyoosheana vidole kwa kutuhumiana.
 
Alisema wajumbe ndiyo wanaoharibu chama na kutengeneza makundi yasiyokuwa na tija.
 
“Ile kamati ya utendaji ya Wilaya iligawanyika kitambo sana, tangu wakati ule wa kuwapata wagombea kupitia viti maalumu, sasa baada ya kuona vile na mpasuko ukizidi kuwa mkubwa, ndiyo kundi moja likamuomba makamu mwenyekiti aje aitishe kikao cha mashauriano cha jimbo.
 
“Sasa kwenye kikao cha usiku ilionekana mpasuko ni mkubwa na hakuna anayeweza kuendesha chama,” alisema mjumbe huyo.
 
Alisema kutokana na malumbano yaliyojitokeza kwenye kujenga hoja baina ya makundi hayo mawili, Mohamed akaamuru kumsimamisha kila mjumbe huku akiwauliza kama wana sababu ya kuendelea kuwapo kwenye nyadhifa zao.
 
Alisema mwisho wa kikao wajumbe hao wakakubaliana kukaa pembeni na kutoa nafasi kufanyika kwa uchunguzi wa kina.
 
Baada ya kamati hiyo kuvuliwa nyadhifa zao, makamu mwenyekti huyo aliamuru ofisi ya chama hicho wilaya iongozwe na madiwani kwa muda wakisaidiwa na uongozi wa chama Mkoa wa Mbeya.
 
Akiendelea kuzungumzia uamuzi huo wa chama Mohamed alisema: 
 
“Kilikuwa kikao cha ndani ya chama ambacho ni siri yetu, hivyo siwezi kukwambia kilichojadiliwa wala hatua zilizochukuliwa. 
 
“Uamuzi wote wa ndani unaamriwa na kumalizwa ndani ya vikao vya kamati ya utendaji, kwa hiyo subiri hadi kamati kuu itakapoamua kuzungumza nje.” 
 
Hata hivyo, Mwambigija alikiri kuondolewa kwa kamati nzima huku akisema chanzo ni makundi yaliyojitokeza kwenye harakati za kumpa mgombea umeya wa Mbeya mjini ndani ya chama hicho.
 
“Nilichokiona, ni kwamba eti nilikuwa upande wa meya aliyepita (Mchungaji David Mwashilindi) hivyo kundi lile ambalo lilishindwa ndiyo limetengeneza zengwe,” alisema Mwambigija.
Post a Comment