Shahidi : Nilimsikia Kubenea akimwambia DC Paul Makonda ni kibaka,mjinga, mpumbavu na cheo chenyewe kapewa. - LEKULE

Breaking

10 Feb 2016

Shahidi : Nilimsikia Kubenea akimwambia DC Paul Makonda ni kibaka,mjinga, mpumbavu na cheo chenyewe kapewa.



Mratibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ASP Denis Mujumba, 39 ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa akiwa Mkuu wa Upelelezi Magomeni alimsikia Mbunge wa Jimbo la Ubungo Saed Kubenea akimwambia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwa DC gani kibaka, mjinga, mpumbavu na cheo chenyewe kapewa.

ASP Mujumba aliyasema hayo  jana mbele ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya kutoa lugha chafu inayomkabili Kubenea dhidi ya Mkuu wa huyo wa Wilaya.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, Mujumba alidai kuwa baada ya Kubenea kuyatoa maneno hayo huku akionekana mwenye hasira, Makonda akiwa amesimama alishangaa, akakunja mikono yake na akawa anamsogelea Kubenea.

“Nikaona watarushiana ngumi, nikamsihi Mkuu wa Wilaya Makonda aondoke wakati huo watu walianza kushangilia huku wengine wakisikitika,” alidai shahidi huyo wa tatu wa upande wa mashtaka.

Alidai kuwa alimgeukia Kubenea na kumwambia kitendo alichofanya cha kutoa matamshi hayo ametenda kosa la jinai, akamkamata na kumpeleka kituo cha polisi Magomeni kwa mahojiano.

Baada ya kutoa ushahidi huo, Wakili wa Kubenea, Peter Kibatala alimuuliza shahidi huyo kuwa ilikuwaje hadi Kubenea akayatamka maneno hayo.

Akijibu swali hilo, Mujumba alidai kuwa ni baada ya Makonda kumnyima nafasi Kubenea ya kuzungumza na wafanyakazi waliokuwa katika mgomo kwenye Kiwanda cha Tooku Garments Co. Limited. 

Pia Wakili Kibatala aliuliza kwamba siku hiyo kulikuwepo na waandishi lakini alipataje picha za video na sauti kutoka kwa waandishi wa habari?

Mujumba: Ni kweli kulikuwepo na waandishi na kwamba niliwasiliana na waandishi hao ili wanipe ushahidi wa picha, sauti au video. Waandishi walinijibu kuwa hawana ushahidi huo.

Kibatala: je ulikwenda na askari wangapi?

Mujumba: nilikwenda na askari wanane au tisa.

Kibatala: wataje majina

Mujumba: Ni Sajenti Peter, PC Hamis, Joachim na Doel.

Kibatala: Shahidi hajui askari wake kwani anajua jina moja tu la mwanzo na hajataja wote.

Maswali haya yalisababisha Mjumba kukunja sura na kutoa sauti ya juu huku akitaka kubishana, Hakimu Simba alimtaka aache kubishana

Wakili Kibatala kwa kutumia sheria Namba 155(a) aliiomba mahakama kuonesha picha za ushahidi zilizokuwa zianonesha hali halisi ya tukio.

Wakili huyo aliinesha mahakama picha ambazo zilionesha kuwepo kwa askari walioshika bunduki na kumzingira Kubena, kwenye picha hiyo Mujumba hakuwemo.

Hapo awali Mujumba aliieleza mahakama kwamba yeye ndiye aliyemsihi Kubenea aende naye kwenye Kituo cha Polisi Magomeni, hivyo Wakili Kibatala aliongeza kuwa, kwa kutokuwepo kwenye picha ile Mujumba alitoa maelezo ya uongo. 

Hakimu Mkazi hata hivyo, baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake, Hakimu Simba alihairisha kesi hiyo hadi tarehe 15 na 16 Aprili mwaka huu.

No comments: