Serikali Ya Zanzibar Yasema Haiko Tayari Kurejea Kwenye Meza Ya Mazungumzo Na CUF Kwa Sasa - LEKULE

Breaking

15 Feb 2016

Serikali Ya Zanzibar Yasema Haiko Tayari Kurejea Kwenye Meza Ya Mazungumzo Na CUF Kwa Sasa



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema hakuna sababu za msingi za kurejewa kwa mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mkwamo wa uchaguzi mkuu wakati Zec tayari imetangaza kufanyika uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu.

Balozi Seif ametoa msimamo huo wa serikali alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Pemba baada ya kumalizika kwa ziara yake ya siku tatu Kisiwani Pemba jana.

Alisema mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar, Dk. Shein na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad,  kuhusu kufutwa kwa uchaguzi mkuu yalifanyika kwa maombi ya Maalim Seif na kwamba mwishowe yeye binafsi akaamua kujiondoka kwenye maendeleo ya vikao vya mazungumzo hayo.

"Kinacholikabili taifa kwa wakati huu ni suala la marejeo ya uchaguzi si njia nyingine, walioamua kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio ni vema wakabakia nyumbani ili kutoa fursa kwa wenzao kushiriki kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowataka," alisema.

Balozi Seif alisema hata kwa upande wake anaheshimu maamuzi ya Zec ambayo hayawezi kuingiliwa na chombo chochote licha ya kwamba tayari alikuwa ameshashinda Jimbo la Mohanda na kupewa cheti kinachothibitisha kuwa mwakilishi wake.

“Tupo tuliokwishashinda kwenye chaguzi zetu za majimbo na kupewa vyeti vinavyotuthibitisha, lakini baadhi yetu kwa nini tuendelee kushutumu maamuzi ya tume ambayo kutokana na sababu za msingi imeeleza kulijitokeza dosari kadhaa kwenye zoezi zima na kulazimika kufuta matokeo na uchaguzi wote,” alisema Balozi Seif.

Akizungumzia uvumi uliojitokeza wa kuwapo kikundi cha vijana wanaopiga watu katika badhi ya maeneo maarufu kama 'Mazombi', Balozi Seif alisema hana taarifa yoyote iliyomfikia akiwa kama kiongozi wa juu wa serikali kuhusu shutma hizo.

Hata hivyo, alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi dhidi ya shutuma hizo na pale itakapobainika kuwapo kwa vitendo hivyo, juhudi za kuwakamata wahusika zichukuliwe na kuwafikisha mbele ya sheria.

No comments: