Mwakyembe: Katiba Mpya sio Kipaumbele cha Rais Magufuli....Wanaofikiri Tutaanza Na Rasimu Ya Warioba Wanapoteza Muda - LEKULE

Breaking

25 Feb 2016

Mwakyembe: Katiba Mpya sio Kipaumbele cha Rais Magufuli....Wanaofikiri Tutaanza Na Rasimu Ya Warioba Wanapoteza Muda



Dr. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria amewataka Watanzania wanaoulizia hatima ya mchakato wa katiba mpya kutambua kuwa suala hilo si sehemu ya vipaumbele vya Dk. John Magufuli.

Mwakyembe amesema hayo jana usiku katika mahojiano maalum aliyofanya na Marin Hassan, mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), juu ya utendaji wa wizara yake katika siku 100 za serikali ya awamu ya tano.

Waziri huyo alisema kuwa katiba mpya haina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku ya watu na wala sio kipaumbele cha rais Magufuli kwani ni kiporo tu alichoachiwa na serikali ya awamu ya nne na atakifanyia kazi wakati atakapoona inafaa.

“Watu wanadhani katiba mpya ndiyo kila kitu, wanaona katiba ni muhimu kuliko kulipia watoto waende shule, wanafikiri katiba mpya ikishapitishwa tu basi kesho yake wataletewa mkate na chai kitandani jambo ambalo sio kweli,” amesema Dk. Mwakyembe.

Aliongeza kuwa: “Kwa sasa rais bado anafanyia kazi vipaumbele vyake kwanza ikiwemo kusimamia elimu bure, kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya serikali na kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma na hivyo kelele za katiba mpya hazina msingi.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe alisema Watanzania ambao bado wana ndoto kuwa mchakato wa katiba mpya unaweza kuanzia katika hatua ya kujadiliwa kwa rasimu ya katiba ya Jaji Joseph Warioba kuachana na wazo hilo kwani limepitwa na wakati.

Alisisitiza kuwa katiba iliyopendekezwa na kupitishwa na wajumbe wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni halali kwani ilipatikana kwa mujibu wa sheria na taratibu licha ya kususiwa na wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ukawa unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), National League for Demokracy (NLD) na NCCR Mageuzi.

“Rais alishasema alipohutubia bunge, kwamba kuna kiporo nimeachiwa, sasa mimi nashangaa hawa watu! tena wengine wana shahada za sheria, wanaongea nini? Hatua ya rasimu ya Warioba ilishapitwa na wakati na tayari tunayo katiba pendekezwa,” aling’aka.

Mwakyembe alihitimisha kwamba utakapofika wakati wa kulifanyia kazi suala la katiba mpya, serikali ya awamu ya tano itaendelea na hatua ya kura ya maoni ya katiba pendekezwa na sio vinginevyo.

No comments: