Mungai Arejesha Serikalini Ardhi Aliyokuwa Amejimilikisha Kinyemela - LEKULE

Breaking

21 Feb 2016

Mungai Arejesha Serikalini Ardhi Aliyokuwa Amejimilikisha Kinyemela


Waziri zamani, Joseph Mungai amerejesha sehemu ya ardhi ya Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, aliyodaiwa kuihodhi kinyume cha sheria.

Baada ya hatua hiyo ya Mungai ambaye aliwahi pia kuwa Mbunge wa Mufindi, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dk Hamisi Kigwangalla ametoa siku saba kwa uongozi wa hospitali hiyo kujenga uzio ili kulinda mipaka yake.

Pia, ameutaka kupeleka ofisini kwake, ramani ya eneo lote la hospitali hiyo na taarifa itakayobainisha kumalizika kwa mgogoro huo.

“Haya ni mambo ya kisheria, isije ikawa leo mnasema mgogoro umekwisha halafu kesho tukasikia mzee Mungai kaenda mahakamani,”alisema Dk Kigwangalla.

Alizitaka halmashauri zote nchini kulinda maeneo yake kwa kuhakikisha yamesajiliwa na yana hati ili inapokuja mipango ya kuboresha au kutanua matumizi kusiwapo na changamoto.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jowika Kasunga alitoa taarifa ya kurejeshwa kwa eneo hilo na kusema lipo nyuma ya hospitali hiyo, mjini Mafinga.

Akizungumzia mipaka ya kiwanja cha hospitali hiyo baada ya waziri huyo kutaka kujua kama haijakumbwa na uvamizi kutoka kwa wananchi, Kasunga alisema eneo hilo lilikuwa na mgogoro wa muda mrefu baada ya Mungai kudai analimiliki kihalali.

Hata hivyo, alisema mgogoro huo umemalizika baada ya Mungai kuamua kulirejesha hospitalini.

Mbunge wa Mafinga Majini, Cosato Chumi alisema eneo hilo lilitengwa kwa  ajili majengo ya uzazi.

“Nashukuru mzee wetu ameamua kulirejesha eneo hilo na sasa lipo mikononi mwa Serikali,” alisema Chumi.

Katika hatua nyingine, Dk Kigwangalla alitoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Shaibu Nnunduma kukamilisha ukarabati wa vyumba vya upasuaji ambavyo hali yake ni mbaya vinginevyo, atatumbuliwa jipu.

Alisema kama angetembelea hospitali hiyo akiwa mkaguzi, angelazimika kufunga vyumba hivyo kutokana na hali yake kutoridhisha.

“Nimekagua na kujionea hospitali hii, kuna maeneo ya changamoto ikiwamo vyumba vyake vya upasuaji, nyie mnaona kama mnavyo lakini kiukweli ni kama hamna kwani vilivyopo vinafanana na stoo, siyo kipimo chake,” alisema Dk Kigwangalla.

No comments: