Chama cha ACT Wazalendo Chamvua Uanachama Ofisa Mipango Na Aliyekuwa Mgombea Urais Zanzibar Kwa Kuhudhuria Vikao Vya ZEC - LEKULE

Breaking

21 Feb 2016

Chama cha ACT Wazalendo Chamvua Uanachama Ofisa Mipango Na Aliyekuwa Mgombea Urais Zanzibar Kwa Kuhudhuria Vikao Vya ZEC



Chama cha ACT Wazalendo kimemsimamisha uanachama Ofisa Mipango wake, Ali Makame Issa kwa madai ya kukiuka maadili ya chama hicho.

Hata hivyo, Issa alisema jana kuwa hajapokea taarifa yoyote kutoka katika chama hicho.

Hatua hiyo dhidi ya kiongozi huyo mwandamizi ndani ya ACT, imekuja baada ya chama hicho kudai kuwa alishirikiana na aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, Khamis Iddi Lila kuwahujumu.

Awali, Lila alisimamishwa uanachama kwa madai ya kutoa misimamo ya kushiriki uchaguzi wa marudio uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha.

Barua ya ACT, iliyosainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Juma Said Sanani imesema: “Kamati maalumu ya Zanzibar imekusimamisha rasmi uanachama kwa mujibu wa katiba ya ACT Ibara ya 11 (2) kuanzia leo Februari 19, 2016, kwa ukiukwaji mkubwa wa katiba Ibara ya 7 (3)(5)(9) Ibara ya 10 (2)(c) (d), Ibara ya 22 (1) (2) (4).”

Barua hiyo inabainisha kuwa mwanachama huyo amekiuka kanuni na maadili pamoja na kukidhalilisha chama.

“Huku ni kukiingiza chama katika mgogoro kwa kuandika barua ya kushiriki uchaguzi wa marudio na kuhudhuria katika kikao cha Tume ya Uchaguzi Februari 17 ukijua kuwa chama kimeshapeleka barua Febuari 9 ya kutoshiriki uchaguzi,” inaeleza.

Vyama vilivyowachukulia hatua viongozi wake kwa madai ya kukiuka kanuni ni Sauti ya Umma (SAU), kilichomfukuza aliyekuwa mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Issa Mohamed Zonga, huku Alliance for Democratic Changes (ADC) kikimfukuza aliyekuwa mlezi wake, Hamad Rashid Mohamed

No comments: