Meneja Vipindi wa kituo cha televisheni cha East Africa (EATV) Afikishwa Mahakamani Kwa Kuhifadhi Raia Wa Kigeni - LEKULE

Breaking

27 Feb 2016

Meneja Vipindi wa kituo cha televisheni cha East Africa (EATV) Afikishwa Mahakamani Kwa Kuhifadhi Raia Wa Kigeni



WATU wawili akiwemo Meneja Vipindi wa kituo cha televisheni cha East Africa (EATV), Lidya Igarabuza (37) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kuishi nchini bila kibali.

Igarabuza ambaye ni mtanzania na raia wa Kenya, David Wachila (36), ambaye anadaiwa kuwa ni DJ wa muziki katika kituo hicho cha televisheni, walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkazi, Kwey Rusema.

Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Khadija Masoud alidai kuwa Februari 25, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni A, Wachila akiwa raia wa Kenya, alikutwa akiishi nchini bila kibali jambo ambalo ni kinyume cha Sheria za Uhamiaji. Katika mashitaka yanayomkabili, Igarabuza anadaiwa kumhifadhi Wachila jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Inadaiwa Februari 25, mwaka huu huko maeneo ya Mikocheni, Igarabuza alikutwa amemhifadhi Wachila huku akijua jambo hilo ni kinyume cha sheria. Washitakiwa walikiri kutenda makosa hayo.

Wakili Masoud aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali. Hakimu Rusema aliahirisha kesi hiyo hadi Machi Mosi, mwaka huu. Igarabuza aliachiwa kwa dhamana wakati mshitakiwa Wachila akirudishwa rumande kwa kukosa wadhamini.

No comments: