Majambazi ambao idadi yao haikufahamika wakiwa na mabomu na bunduki za kisasa jana walivamia Benki ya Access tawi la Mbagala ambako walipora viroba vya fedha, kuua mlinzi na baadae wanne kati yao waliuawa na jeshi la polisi.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema baada ya majambazi hao kufika katika benki hiyo kwa bodaboda nne majira ya saa nane mchana,yalimuua mlinzi wa benki hiyo, kusha kubomoa kwa risasi mlango wa vioo na kuingia ndani na kuzua taharuki kubwa
Mashuhuda hao walisema, katika tukio hilo lililodumu kwa karibu saa moja,mmoja wa majambazi hao aliyekuwa amevaa kininja,alikuwa barabarani akiamuru magari kupita haraka huku akifyatua risasi hovyo.
Ilielezwa kuwa, jambazi huyo aliyeonekana kuwa na uzoefu wa matumizi ya bunduki alikuwa akifyatua risasi kwa kutumia mkono mmoja na ndiye aliyewajeruhi baadhi ya wapita njia.
Hivyo,wakati uporaji ukiendelea na jambazi huyo akiimarisha ulinzi barabarani baadae hakukuwa na magari wala pikipiki zilizokuwa zikipita.
Mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi jirani na benki hiyo,Ramadhani Tairo alisema baada ya jambazi huyo kuliona gari la polisi likielekea eneo la tukio,alifyatua risasi na kulipiga kabla halijafika.Gari hilo lilipoteza mwelekeo na kutumbukia mtaroni.
Tairo alisema mbali na jambazi huyo kulipiga risasi gari la polisi pia alilirushia bomu la mkono,lakini liliangukia barabarani bila kuripuka.Polisi walifanikiwa kulilipua bomu hilo baadae likiwa halijasababisha madhara kwa wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo.
Mkazi mwingine wa eneo hilo,Rebecca Maliva alisema majambazi walioingia ndani ya benki hiyo walioneka wakitoka na viroba vitatu vya fedha ambavyo walivipakata kwenye pikipiki na kuondoka kwa kasi kuelekea Mkuranga kupitia barabara ya Kilwa.
Rebecca alisema polisi zaidi walifika kwenye eneo hilo wengine wakiwa kwenye pikipiki na kuanza kuwafukuza majambazi hao ambapo walipofika eneo la shule ya St. Marry's,walitupa kiroba kimoja cha fedha ambacho wananchi waliokuwa jirani waligombania na kuchukua fedha zilizokuwemo na kisha kila mmoja kukimbia na burungutu la noti.
Baada ya nusu saa wakati umati ukiwa bado upo kwenye benki hiyo,magari ya polisi yalipita katika eneo hilo yakitokea eneo la Mkuranga yakiwa yamebeba miili ya majambazi yaliyouawa.
Magari hayo yalikuwa yakisindikizwa na vijana wa bodaboda waliokuwa wakishangilia kazi iliyofanywa na polisi.
Kamanda wa p[olisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alizungumzia kwa ufupi tukio hilo n kwamba majambazi manne yaliuawa na kukamata silaha tatu,lakini hakutaka kuingia kwa ndani akisema atatoa taarifa zaidi leo
No comments:
Post a Comment