Maandamano ya Kupinga Uchaguzi wa Marudio Zanzibar Kufanyika Bukoba - LEKULE

Breaking

27 Feb 2016

Maandamano ya Kupinga Uchaguzi wa Marudio Zanzibar Kufanyika Bukoba



CHAMA cha Wananchi (CUF) Bukoba kimejiandaa kufanya maandamano ya amani keshokutwa, kwa ajili ya kupinga kufanyika upya uchaguzi wa Zanzibar unaotarajiwa kuwa Machi mwaka huu.

Kimeiomba pia serikali ya awamu ya tano, kuchukua uamuzi wa kumtambua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais Zanzibar na kuwa hakiko tayari kurudia uchaguzi huo tena.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama hicho, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Saverina Mwijage, alisisitiza kuwa kamwe chama hicho hakitakuwa tayari kurudia uchaguzi huo uliotangazwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa utafanyika Machi 20,kwa kile kinachodaiwa ni kufutwa uchaguzi wa Oktoba 25,mwaka jana.

“Tumedhamiria kuandamana ili kumfikishia ujumbe wetu Rais John Magufuli kupitia kwa Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella lengo letu hasa ni kupinga uchaguzi wa Zanzibar. Hali ya Zanzibar kwa sasa haiko shwari, watu wanatishiwa maisha yao, wanaishi kwa hofu juu ya maisha,” alisisitiza.

Mwijage ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF Taifa, alisema chama hicho kinatambua uchaguzi ulishakwisha na tume hiyo ilishatoa vyeti kwa walioshinda, kwa mantiki hiyo CUF inamtambua Maalim Seif kuwa alishinda katika uchaguzi huo.

Alisema maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri na baadaye utakuwepo mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mayunga ulioko mjini Bukoba ili kuutangazia umma juu ya msimamo wa chama hicho na baada ya hapo watazunguka katika wilaya za Muleba, Missenyi na Karagwe.


No comments: